Jinsi Nakuru ilivyoukaribisha Mwaka Mpya 2021

Jinsi Nakuru ilivyoukaribisha Mwaka Mpya 2021

Na RICHARD MAOSI

WAKAZI wengi wa Nakuru walilazimika kusalia majumbani mwao usiku wa Desemba 31, 2020, kukaribisha Mwaka Mpya 2021.

Kinyume na mwaka uliopita sherehe za mwaka huu zilikosa mbwembwe, jamaa na marafiki wakikosa fursa ya kutembeleana na kujuliana hali.

Polisi walishika doria katika barabara kuu za kuingia na kutoka mjini Nakuru kama vile Kenyatta, Moi na Gusii road ili kuhakikisha kumbi za burudani zinasalia kufungwa na watu wanaheshimu sheria za kafyu.

Kamanda wa polisi kutoka Nakuru Mashariki Bi Elena Kabukuru, alisema kuwa operesheni hiyo ililenga kunasa wale waliokuwa wakikaidi agizo la kutotoka nje usiku.

Kaunti ya Nakuru haikushuhudia idadi kubwa ya wageni mwaka huu, jambo lililofanya shughuli za biashara kushuka.

Kinyume na siku za mbeleni ambapo watu wengi walihudhuria ibada ya kesha, mambo yalikuwa tofauti mkesha wa 2020 makanisa yakisalia kufungwa.

Mkesha wa kukaribisha Mwaka Mpya 2021 mjini Nakuru huku polisi wakiendelea kushika doria katika barabara kuu za kutoka na kuingia mjini humo. Picha/ Richard Maosi

Kulingana na Kabukuru kabla ya usiku wa manane polisi walikuwa wamekamata jumla ya magari tano na watu kadhaa waliopatikana wakizurura usiku.

Hata hivyo Taifa Leo ilibaini kwamba waendeshaji teksi na bodaboda nje ya mji wa Nakuru walipandisha nauli na kuendelea kusafirisha walevi.

Aidha kilabu maarufu cha 7D Platinum kilichoko katika barabara ya Nakuru-Nairobi kilifurika wateja, huku wakiendelea kupata burudani na kupuuza kanuni za kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Vile vile makahaba katika barabara ya Gusii waliendelea kutafuta wateja.

Mitaa ya Kaptembwa, Freehold, Langalanga, Rhonda na London ilishuhudia umati mkubwa wa watu waliowasha moto barabarani wakisubiri kukaribisha Mwaka Mpya usiku huo.

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Dhana na dhima ya malipo na ada...

Wakulima, wafugaji wataka usaidizi wa serikali