Makala

Jinsi niliponyoka mauti mikononi mwa kakangu wa kambo aliyeua mpenzi wangu

April 11th, 2024 4 min read

RUSHDIE OUDIA na CHARLES WASONGA

AKILALA kwenye sakafu baridi ya nyumba yake, ya vyumba viwili vya kulala katika mtaa wa Migosi, Kisumu, Evans Aloyo Otieno alijua kuwa angekufa baada ya muda mfupi.

Hata hivyo, katika hali kama hiyo, alijiambia kuwa hangekufa kabla ya kakake wa kambo, Joseph Ayomo, aliyekuwa akimshambulia, kumwambia sababu za kumtendea ukatili huo.

“Mbona unaniua,” alimuuliza Ayomo mara kadhaa ambapo alijibu hivi: “Hautajua lakini sharti ufe”.

Huku akishawishika kuwa alikuwa amemmaliza, Ayomo aliamka na kutembea kwa hatua chache na kuwasha msokoto wa bangi aliyovuta akitembea huku na kule.

Bw Otieno, ambaye alikuwa akijifanya amekufa wakati huo, alimtazama kwa ukaribu.

Katika uamuzi wake, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Winam Bw Robert Oanda alitaja kunusurika kifo kwa Bw Otieno kama “mkono wa Mungu na maajabu”.

Kauli sawa na hiyo ilitolewa na wahudumu wa afya katika Hospitali ya Avenue waliomhudumia Otieno baada ya majirani zake kumkimbiza huko.

“Hata daktari mpasualji aliyenishughulikia hakuamini kuwa niliponea kifo,” akasema Bw Otieno.

Kisa hicho cha kuogofya kilifanyika 2018.

Kakake wa kambo

Bw Otieno, aliyekuwa mwenye umri wa miaka 33, alikuwa akiishi na kakake wa kambo, mdogo, Joseph Ayomo, 23.

“Nilipohamia Kisumu kutoka Nairobi, nilimwomba kakangu aje tuishi naye kwa sababu nyumba ilikuwa kubwa zaidi. Alikuwa akiishi na dada zake katika mtaa mmoja na hakuwa na ajira yoyote kwa sababu alikuwa angali mwanafunzi wa chuo kikuu,” Bw Otieno akaeleza.

Kaka wawili waliishi pamoja kwa amani kwa karibu mwezi mmoja.

“Mahusiano yetu yalikuwa mazuri na tulishiriki chakula pamoja nikiwepo nyumbani. Tungezungumza mara chache kwa sababu nilikuwa nikisafiri kila mara kwa shughuli za kibiashara. Nilikuwa nimempa ufunguo wa ziada wa nyumba,” akasema Bw Otieno.

Siku ya tukio, Otieno anakumbuka jinsi alimuaga kakake na mpenziwe (Otieno) Beverly Akinyi ambaye aliishi Nairobi lakini aliwatembelea kuwajulia hali.

Beverly, 21, alikuwa mwanafunzi wa Mwaka wa Kwanza katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Aliondoka kwa gari lake aina ya Toyota Noah.

“Wakati fulani mchana huo nilimpigia simu Beverly kumjulia hali lakini singeweza kumfikia. Lakini sikuwa na wasiwasi kwa sababu ilikuwa jambo la kawaida kwa simu yake kuzimwa,” Bw Otieno akaeleza.

Alifunga duka lake, lililokuwa katikati mwa jiji la Kisumu, mwendo wa saa moja za usiku na akaelekea nyumbani. Alipitia duka la supermarket, ambako alinunua mboga na mahitaji mengine ya kimsingi.

Aliwasili nyumbani dakika chache kabla ya saa mbili za usiku.

Kakake Ayomo akafungua mlango.

Uamuzi wa Hakimu Mkazi Winam

Kulingana na uamuzi uliotolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Winam, ilisemekana kuwa baada ya kaka hao wawili kusemezana, Bw Ayomo alirejea sebuleni ambako alikuwa akitizama filamu fulani kwenye runinga huku Otieno akielekea jikoni akibeba vitunguu alivyonunua.

Hata hivyo, kabla ya Otieno kupiga hatua ya pili aligongwa kwa nguvu nyuma ya kichwa, akaanguka sakafuni na kuzirai.

Baadaye Bw Otieno aliamshwa na uchungu makali mgongoni mwake.

Alipopata fahamu, aligundua kuwa kakake wa kambo alikuwa amemkalia kiunoni huku akimdunga mara kadha kwa kisu cha jikoni.

“Nilipambana naye na katika harakati hizo akanidunga kisu kwenye mikono yangu ya kulia na kushoto, mara kadha,” akaeleza.

Alisitisha shambulio hilo baada ya kisu hicho kuvunjika mara mbili.

Lakini katika mapambano hayo, Bw Otieno hakukosa kujiuliza aliko mpenziwe Beverly.

Hakujua kuwa mwili wa Beverly ulikuwa mita chache karibu na mahala ambapo alikuwa akipambana na kakake.

Anakumbuka kugusa mwili huo kwa mguu wake usiku huo akipambana na kaka huyo hali iliyomfanya kugundua kuwa Ayomo alikuwa akinuia kumuua.

Bw Otieno baadaye alisema alimwona kakake akibeba mwili wa Beverly kutoka chumba cha kulala hadi nje ya nyumba.

Ayomo alipoondoka, alipanda kitandani kwa sababu “sikutaka kufa kwenye sakafu baridi.”

Lakini Ayomo aliporejea na kumpata kitandani, alichukua kifaa butu na kupiga tena hadi akaanguka sakafuni.

“Nilibingiria haraka mvunguni mwa kitanda hadi ikawa vigumu kwake kunishambulia,” Otieno akaeleza.

Hata hivyo, hii haikudumu kwa muda mrefu kwani Ayomo alikamata miguu yake na kumburuta nje.

“Alitia vidole vyake ndani ya mdomo wangu katika jaribio la kunikosesha hewa. Pia alijaribu kunyofoa macho yangu lakini hakufaulu,” Bw Otieno akaeleza.

Ajifanya amekufa

Kwa mara ya pili akitendewa ukatili huo, alijifanya amekufa.

Kwa mara nyingine, Ayomo alipima mdundo wa moyo wa kakake na akaonekana kushawishika kuwa kweli alikufa.

Kulingana na Bw Otieno, kakake muuaji alipekua mifuko yake na kuchukua ufungua wa gari lake na simu yake na rununu. Aidha, alimvua mavazi yake yaliyokuwa yamelowa damu na kufunga kwa shiti ya kitanda.

Baadaye Ayomo alimbeba Otieno hadi kwenye gari ambako mwili wa Beverly ulikuwa umewekwa katika kiti cha nyuma.

Lakini Otieno alibahatika pale kakake aliporejea chumbani orofa ya juu kusafisha uchafu.

“Nilijua kuwa hii ilikuwa nafasi yangu ya mwisho kuokoa maisha yangu. Nilijipiga moyo konde na kufungua mlango wa gari na kuondoka nje. Nilijikokota hadi nikafika katika mlango wa mmoja wa majirani zangu na nikabisha kwa nguvu zote nilizosalia nazo. Nilienda katika nyumba nyingine na kugonga dirisha la chumba cha kulala hadi kioo kikavunjika. Majirani wakapiga kamsa,” akaeleza.

Katika harakati hizo, mshambuliaji aliponyoka na kutoroka kwa miguu.

Baadaye, Bw Otieno aligundua kuwa Ayomo alienda kwa nyumba ya dadake iliyoko karibu.

Alimwambia dadake kwamba alikuwa ameshambuliwa na wakora huku akielezea chanzo na alama za damu katika mavazi yake.

Hatua ya haraka ya wahudumu wa afya katika Hospitali ya Avenue ilimnusuru Bw Otieno kutoka na shambulio hilo.

Miaka sita baada ya shambulio hilo bado humshtua anapoelezea lilivyotekelezwa.

Kulingana na hakimu, Bw Otieno alipona kimiujiza.

Muujiza wa kuponea kifo

“Nakubaliana na mlalamishi kwamba Mungu ndiye alimwezesha kuponea kifo; ilikuwa muujiza. Baada ya kuwasikiza mashahidi wote, na kwa kuzingatia rekodi ya ushahidi, nimeshawishika kuwa mshtakiwa alishiriki katika jaribio la kumuua mlalamishi, kakake wa kambo. Utetezi wake na ushahidi wa dadake yote ni njama ya kufunika ukatili uliotekelezwa na mshtakiwa,” akasema Hakimu Oanda.

Bw Ayomo alipatikana na hatia ya kujaribu kuua na akahukumiwa kifungo cha miaka 20 gerezani.

Akijitetea, mshtakiwa alisema anajutia kosa hilo na kuiomba mahakama imhukumu kifungo cha nje kwani mamake anaugua saratani na anahitaji kumhudumia.

Mahakama ilikataa ombi hilo.

Bw Ayomo anasubiri hukumu nyingine mnamo Aprili 16, 2024 baada ya mahakama kumpata na hatia ya kumuua Beverly Akinyi.

Lakini huku akisubiri haki, Bw Otieno bado anajizatiti kuelewa ni kwa nini kakake wa kambo alitaka kumuua baada ya kumuua mpenziwe.