Makala

'Jinsi nilivyofurahia likizo'

September 4th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

ASHLEY Meitamei, 9, anasema likizo – wakati ambapo shule huwa zimefungwa – humpa raha tele katika maisha yake kwa kuwa ndio wakati yeye hupata fursa ya kutembea mashinani kujipa raha nje ya maisha ya mjini.

Ndugu zake anawaorodhesha kama Immaculate, Sisina na Ramsey na ambao anasema anawapenda sana kwa kuwa “ni wa kuzaliwa na wazazi wangu na ni lazima tuwe na upendo kama familia.”

Wakati likizo ikitamatika, alisema ilikuwa ya kufana lakini anafahamu fika kuwa anahitaji masomo kuafikia ndoto zake za kimaisha na hivyo basi kukubali kuwa “kila kitu na wakati wake na sasa ni kutia kikomo raha za likizo na kurejelea masomo yangu.”

Akiwa ni mzawa wa Kaunti ya Kajiado kwa familia ya Elizabeth Njeri Muiruri na Daniel Leshau Solio, kijana huyu anasema jijini huwa hapati nafasi ya kucheza na mbwa, mbuzi, kuku na hata ng’ombe.

Ashley Meitamei. Picha/ Mwangi Muiruri

“Kwetu hata hakuna nafasi ya kuogelea kwa mto, lakini nikienda kwa shosh’ na gukaa (nyanya na babu) katika Kaunti ya Murang’a, ni kufurahia maisha,” asema.

Meitamei ambaye hushikilia kuwa angetaka kuwa mkuu wa kanisa lake ili awe akiwapa afueni na wokovu watu waliopagawa pepo anasema anapenda sana kushuhudia chakula kikipikwa kwa kutumia jiko la kienyeji la kutumia kuni, kunywa chai kwa vikombe vya mabati na kula chakula akitumia vidole vya mikono iliyonawishwa.

Mcheshi ajabu, aliye mwingi wa roho ya usafi wa watoto, Meitamei anasema chai ya mashambani huwa na sukari nyingi kushinda ya mjini.

Anapenda githeri (pure) ambapo anasema kwake ni chakula kitamu kuliko Spaghetti za mjini na angepewa nafasi ya kujiamulia, angechagua kubakia mashambani na asajiliwe katika shule ya msingi ya umma ili awe na nafasi ya kucheza na watoto wengine.

“Huku mashambani kila mahali ni uwanja wa kuchezea. Ukiingia shambani kuna miti ya kuparaga na kurukia; kuna hata tumbili wa kukimbiza pamoja na mbwa wa mjomba wangu na watoto wa kucheza nao ni wengi sana,” asema.

Anasema kuwa mashambani kwao huko hakuna kelele za mijini ya walevi wakipiga mayowe, wengine wakishangilia michuano ya kabumbu na wengine wakikorofishana tu.

Anasema raha yake mashambani tena hutokea katika hali kwamba maafisa wa polisi si wengi sana kwani “naogopa bunduki kwa hakika.”

Meitamei anasema huko kuna amani.

“Unapendwa na watu wengi kama wajomba, shangazi, majirani wanaotaka kukujulia hali na katika awamu nyingi za shughuli, huwa na maombi tele,” asema.

Anasema kuwa hakuna kitu humpendeza zaidi kama kushiriki maombi na nyimbo na kupiga stori na wanakijiji.

Kijana huyu anasema kuwa isipokuwa ni vile nyakati zingine hukosa ndugu yake mdogo na dada zake wawili, ambao mara kwa mara huwa wako Kajiado, yeye akikimbizana na mbuzi mashambani, anaona mashinani kuwa ni kuzuri sana.

“Kuna maombi, wengi hujua nyimbo za Mungu na wengi pia husoma Biblia. Unaambia Mungu akubariki na wengi na katika hali nyingi, unasikia wanakijiji wakisema Mungu yuko katika kiti chake cha enzi,” asema.

Meitamei anasema kuwa akishakuwa mkubwa, anawazia kujinunulia kipande cha ardhi katika eneo moja kijijini na ajijengee nyumba na alee familia yake katika utulivu na raha mashinani kando na hekaheka mijini ambako pia anasema kuna kila aina ya hatari kuhusu uchafuzi wa mazingira, uhalifu na magonjwa kando na gharama za juu za maisha.

Anasema mashujaa wake ni mamake mzazi na babake mzazi “ambao walinizaa na wanaendelea kunilea wakinipa ushauri wa kimaisha na kunionyesha mapenzi na la mno, kunifundisha nimtambue na nimpende Mungu kama tegemeo langu na letu katika maisha.”