Habari MsetoSiasa

Jinsi nilivyomwokoa Moi alipostaafu – Francis ole Kaparo

February 10th, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

ALIYEKUWA Spika wa Bunge Francis Ole Kaparo amefichua alivyomnusuru Rais Mstaafu Daniel arap Moi dhidi ya kufurushwa kutoka katika jumba la Kabarnet Gardens baada ya kustaafu 2002.

Mara baada ya Rais Mwai Kibaki kuapishwa, baadhi ya viongozi wa chama tawala cha NARC walitaka kumfurusha Mzee Moi kugura kutoka katika jumba hilo amwachie Michael Kijana Wamalwa aliyekuwa makamu wa rais.

Jumba la Kabarnet lililoko karibu na mtaa wa mabanda wa Kibera jijini Nairobi, lilikuwa likitumika kama makao ya manaibu wa rais wakati wa utawala wa Mzee Jomo Kenyatta.

Manaibu wa rais waliotangulia Moi; Jaramogi Oginga Odinga na Joseph Murumbi waliishi katika jumba hilo.

Moi aliingia kwenye nyumba hiyo Mzee Kenyatta alipomteua kuwa makamu wa rais wa tatu mnamo 1967.

Baada ya kifo cha Jomo Kenyatta, Rais Moi alienda kuishi Ikulu lakini akakataa kumwachia makamu wake Mwai Kibaki jumba la Kabarnet.

Hatimaye Rais Moi aligeuza jumba hilo kuwa makao yake ya kibinafsi.

Kulingana na mwendesha shughuli za ikulu wa zamani Franklin Bett, Moi alifanyia kazi Ikulu lakini jioni alienda kulala katika jumba la Kabarnet.

Lakini Rais Mwai Kibaki alipochukua hatamu za uongozi, chama cha Narc kilianza juhudi za kutaka kumfurusha Mzee Moi kwa nguvu.

“Katibu wa kibinafsi wa Mzee Moi, John Lokorio alinipigia simu kunifahamisha kwamba serikali ilitaka kumfurusha Rais Mstaafu. Nilimwendea Rais Kibaki nikamsihi asimpokonye Mzee Moi jumba hilo,” akasema Bw Kaparo ambaye alikuwa spika wa Bunge wakati huo.

“Nilimwambia Rais Kibaki kuwa aache Mzee Moi astaafu kwa amani. Baadaye niliwakutanisha viongozi wawili hao katika mkutano wa faragha. Hapo ndipo Rais Kibaki alikubali Mzee Moi apewe hati miliki ya nyumba ya Kabarnet,” akaongezea.

Alisema Rais Mstaafu Moi na Rais Kibaki walionekana pamoja hadharani katika harusi ya mtoto wake mnamo 2004. Baada ya mwafaka huo, serikali ya Kibaki iliamua kujenga jumba jingine la makazi ya naibu wa rais katika mtaa wa Karen kwa kutumia Sh 383 milioni mnamo 2005.

Naibu wa Rais William Ruto ndiye naibu wa rais wa kwanza kuishi katika makazi hayo mapya.

Bw Kaparo pia alisimulia jinsi Mzee Moi alimwezesha kuwa spika.

“Nilikuwa wakili katika eneo la Nyeri nikitetea wakulima. Wakati huo, maskini walikuwa wakidhulumiwa katika ununuzi wa mashamba. Baada ya juhudi za kuwatafutia haki mahakamani na polisi kugonga mwamba. Niliamua kumwandikia barua Rais Moi japo hakunijua na wala sikuwa nimewahi kukutana naye,” akaelezea.

Barua hiyo ilimfikia Rais Moi akatuma polisi kwenye kumchukua Bw Kaparo kumpeleka Eldoret kukutana naye.

“Nilishtuka nikidhani kwamba nimekamatwa, lakini nilipofika Eldoret niliona Mzee Moi akitabasamu. Nilimsimulia kuhusu masaibu ya wakulima na akaaunda tume,” akasema Bw Kaparo aliyeongoza Bunge kati ya 1993 na 2008.

“Nilipojitosa kwenye siasa, Rais Moi aliniteua kuwa Waziri Msaidizi wa Masuala ya Kisiasa. Uchaguzi ulipofika niliwania kiti cha ubunge cha Laikipia Mashariki nikabwagwa. Nikajiondoa kwenye siasa. Lakini Mzee Moi aliniita na kuniambia kwamba mimi ndiye nitakuwa spika wa Bunge,”alisimulia.