Siasa

Jinsi njama ya kuua Azimio ilivyotibuka

May 10th, 2024 2 min read

NA COLLINS OMULO

MABADILIKO ya kisiri yaliyofanyiwa miswada ya kufanikisha utekelezaji wa ripoti ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (Nadco) iliyowasilishwa majuzi katika Seneti yalifuchua njama fiche ya kuvunja Azimio la Umoja-One Kenya.

Imegundulika kuwa kulikuwa na njama iliyopangwa na mrengo wa Kenya Kwanza, unaoongozwa na Rais William Ruto, kwa mfano, kufanya mabadiliko katika Mswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2024 ili kufutilia mbali vyama vya miungano.

Hatua hiyo ingeua kabisa muungano wa Azimio unaoongozwa na Raila Odinga, ambayo inatambuliwa kama chama cha kisiasa na muungano wa vyama, kwa wakati mmoja.

Njama hiyo ilitibuliwa wiki hii na Kiongozi wa Wachache katika Seneti Stewart Madzayo aliyewasilisha malalamishi kwa Spika Amason Kingi ambaye aliamuru kuondolewa kwa mswada huo baada ya kuwasilishwa na Kiongozi wa Wengi Aaron Cheruiyot.

Bw Madzayo, ambaye ni Seneta wa Kilifi, alisema hatua ya mrengo wa Kenya Kwanza kupendekeza kuwa Sheria ya Marekebisho ya Vyama vya Kisiasa ya 2022 ifanyiwe marekebisho kwa kuondoa kiashirio, “chama cha muungano wa vyama vya kisiasa,” ingeua Azimio kabisa “pamoja na haki na manufaa yote inayopata bungeni na katika sheria.

“Azimio ndicho chama cha muungano cha kipekee nchini na ukiondoa kiashirio hicho, basi unalenga Azimio. Ikiwa mswada huo ungepitishwa ulivyokuwa, Azimio haingekuwepo tena. Tungerejesha taifa hili katika utawala wa chama kimoja,”akaeleza Seneta Madzayo, ambaye ni mwanasheria na jaji mstaafu.

Ili kuzuia kufufuka kwa Azimio, mrengo wa Kenya Kwanza pia ulijaribu kupendekeza kufutuliwa mbali kwa sehemu kadhaa katika sheria hiyo ya 2022 zinazohusiana na taratibu za uundaji, usajili, utoaji cheti na uongozi wa chama cha muungano. Aidha, mrengo huo ulitaka hitaji la sheria hiyo kwamba chama cha muungano kiwasilishe stakabadhi ya makubaliano katika afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa kabla au baada ya uchaguzi mkuu liondolewe.

Bw Madzayo alisema hatua hiyo ililenga kuharamisha stakabadhi ya makubaliano kati ya vyama tanzu vya Azimio iliyotiwa saini na kuhifadhiwa kwa afisi ya Msajili Mkuu wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

“Inasikitisha kuwa ukora kama huu unaweza kutokea katika kizazi cha sasa. Watu hawafai kuendesha njama kama hii ikiwa kweli tunaheshimu na kuipa uzito demokrasia yetu,” akasema Seneta Madzayo.

Kenya Kwanza haikukomea hapo katika njama ya kupenyeza mabadiliko “sumu” katika miswada ya kutekeleza ripoti ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (Nadco).

Njama nyingine ni kusudi la kuingilia uendeshaji wa uchaguzi na upeperushaji wa matokeo kieletroniki.

Kuhusiana na Mswada wa Marekebisho ya Uchaguzi ya 2024, Kenya Kwanza ilipenyeza sehemu mpya baada ya sehemu ya 38 katika sheria asilia, inayosema kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itaamua sehemu zitakazotumika kama vituo vya kupigia kura.

Mrengo wa Wengi ulipenyeza mabadiliko mengine ambayo yanalengo kulazimisha IEBC kutambua hata magari au vyombo fulani vya usafiri majini kuwa vituo vya kupigia kura.

Hii ni kinyume na Sehemu 38 A (1) (a) ya sheria ya sasa inayosema kuwa tume hiyo itatenga sehemu fulani katika eneo wakilishi kuwa vituo vya kupigia kura, wala sio vyombo vya uchukuzi.

Kenya Kwanza pia ilifuta maneno ‘Fomu Maalamu’ kutoka sehemu inayohusu uwasilishaji wa matokeo baada ya kutangazwa katika vituo vya kupigia kura. Kulingana na Sehemu ya 39 (4) (b) ya sheria ya sasa, IEBC inapaswa kuwasilisha, kieletroniki, matokeo ya uchaguzi wa urais hadi vituo vya maeneo bunge, kaunti na kituo cha kitaifa saa mbili baada ya kutangazwa katika vituo vya kupigia kura.