Makala

Jinsi nyama ya kasa inavyotayarishwa kuepuka vifo kama vilivyotokea Zanzibar

March 14th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

WENYEJI wa visiwa mbalimbali vya Lamu wameeleza jinsi nyama ya kasa inavyotayarishwa ili kumuepusha mja na sumu au madhara mbalimbali.

Ikumbukwe kuwa kasa ni mnyama wa baharini afananaye na kobe na ambaye huwa na magubiti makubwa.

Kasa huzaa kupitia mayai, ambapo huyataga kwenye nchi kavu, hasa katika fukwe zilizojificha za Bahari Hindi na ambazo zina mchanga mwingi.

Mzee wa kisiwa cha Lamu, ambaye pia hupenda kasa, Bw Mohamed Mbwana, anamtaja mnyama huyo kuwa na minofu tamu isiyolinganishwa au kukadiriwa na wanyama wengine wowote ulimwenguni.

Mzee Mohamed Mbwana kwenye mahojiano na Taifa Leo ambapo alisema utamu wa nyama ya kasa ni kumpika bila kiungo chochote. Aliongeza kwamba kasa ana nyama tamu isiyolinganishwa na mnyama yeyote duniani. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Mbwana aidha anashikilia kuwa huku watu wengi wakikimbilia kutumia viungo vingi wakati wanapoandaa mapishi yanayohusisha nyama, kwa wale wanaopika minofu ya kasa hawana haja ya kubabaika.

Anashikilia kuwa utamu wa kasa ni kumpika bila viungo vyovyote.

Anasema baada ya kumvua kutoka majini, kasa lazima achinjwe kama vile ifanyikavyo kwa mbuzi au ng’ombe.

Hiki ni kinyume kabisa na viumbe wengine wa baharini kama vile samaki.

Kutokana na gamba au ngozi yake ngumu, mchinja na mtayarishaji kasa humpindua kwa chini, kumbambua na kisha kuanza kuitoa minofu yake.

Kasa amebarikiwa na mafuta mengi, hivyo mwenye kuandaa nyama yake lazima awe makini ili asiharibu mapishi yake.

“Hapa utahitajika kutoa viungo vya ndani, ikiwemo maini na matumbo ambayo yamejaa tele mafuta. Baadaye unapaswa kuikatakata nyama kwa makini na kuiosha vizuri. Kisha iweke kwa sufuria na kuanza kuichemsha bila ya kuweka maji. Nyama ya kasa hujipika yenyewe,” anaeleza Bw Mbwana.

Anasisitiza kuwa punde mpishi anapoweka maji kwenye nyama ya kasa, hivyo ndivyo anaiharibu nyama hiyo kwani hulegealegea na kukatikakatika, hivyo kukosa utamu au ladha yoyote.

“Huyu mnyama hupikwa na mafuta yake tu. Baada ya kuosha nyama, itumbukize kwenye sufuria na kufunika itokote kwa angalau dakika 30 hivi. Punde mafuta au unyevunyevu ukikauka, hivyo ndivyo nyama yako iko tayari kupakuliwa mezani. Nyama ya kasa ikipikwa kwa makini ni tamu ajabu,” akasema Bw Mbwana.

Kwa wale ambao hawawezi kupika nyama bila viungo wanashauriwa kutumia kitunguu maji pekee iwapo wana lazima ya kufanya hivyo.

Bw Kassim Shee, mvuvi na mzee wa kisiwa cha Kizingitini, Lamu Mashariki anasema endapo mja hatakuwa makini kwa kutenga vilivyo au kuchuja ipasavyuo mafuta ya kasa huenda yakamdhuru kiafya.

Bw Shee anafafanua kuwa pia ni lazima mtayarishaji nyama ya kasa kuwa na weledi wa kuikata na kuitenga nyongo ya kasa kwani ikitoboka na kutapakaa kwenye nyama, husababisha ladha kuwa chungu kama shubiri.

Isitoshe, Bw Shee anasema lazima wanaomla kasa kufahamu vyema kwamba kuna kasa aina mbili–wale wa kuliwa na wasioliwa.

Kasa wasioliwa wanafahamika kwa jina ng’amba. Huyu ni kasa mwenye magamba kama sandarusi na yanayong’aa.

“Sisi Wabajuni wa Lamu tumesifika kwa uvuvi na tunajua mengi kumhusu huyu kasa,” akasema Bw Shee.

Hivyo anatahadharisha si aina yote ya kasa wanaliwa kama alivyosema mwanzo.

“Punde tunapomnasa kasa mtegoni tayari tunajua iwapo ni wa kuliwa au la. Ikiwa si yule wa kuliwa, basi hatusiti kumnasua kutoka mtegoni na kumrudisha baharini,” akaeleza.

Kulingana na mzee huyu, kasa asiyeliwa ana sumu kali na wao humuita ng’amba.

“Ndipo utapata kwamba watu wamekula kasa na kisha kuishia kulazwa hospitalini huku wengine wakiaga dunia. Ina maana kwamba huwa hao watu hawajamla kasa tunayemjua bali yule ng’amba mwenye sumu kali,” akaeleza.

Kauli ya wakazi wa Lamu kuhusu nyama ya kasa na jinsi inavyopikwa au kutayarishwa kuepuka sumu inajiri wakati ambapo Jumatatu wiki hii Mwananchi ilisema vifo vya watu wanaodaiwa kula nyama ya kasa eneo la Kisiwapanza Wilaya ya Mkoani, Kusini Pemba vilikuwa vimefikia tisa, huku wengine 98 wakilazwa kutokana na tatizo hilo.

Habari za watu kudaiwa kula nyama hiyo mnamo Machi 5, 2024, zilienea kote Afrika Mashariki na taarifa za awali zikaeleza kuwa walioaga dunia walikuwa ni watoto wanane wa chini ya umri wa miaka 10 katika familia sita huku familia moja ikipoteza watoto wawili.

Kasa aliyevuliwa baharini kwa nyavu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Daktari wa Wilaya ya Mkoani, Bakar Haji, alisema mmoja kati ya watu waliolazwa naye alipoteza maisha alipokuwa akiendelea kupokea matibabu.

“Mtu mwingine msichana, Sabrina Makame Khamis (22) pia alifariki dunia, huku wagonjwa 98 wakiwa bado wamelazwa hospitalini,” alisema Dkt Haji.

Kufuatia mkasa huo, wataalamu waliweka kambi ya dharura kwa ajili ya kutoa huduma kwa mtu yeyote mwingine ambaye huenda akajitokeza na dalili za kuathirika.

Dkt Haji alisema ingawa wagonjwa waliongezeka, hali zao zinaendelea vizuri tofauti na siku za mwanzo, huku wakiendelea kufanya uchunguzi na kusubiri majibu ya sampuli kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

Mkuu wa Wilaya ya Chake-Chake anayekaimu nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkoani, Abdalla Rashid Ali, alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuongeza madaktari katika Kituo cha Afya cha Kisiwapanza.

Alisema kwa sasa hali inaendelea vizuri kwani wagonjwa walioongezeka wameshatibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani, huku wengine wakizuiliwa mpaka wataalamu watakapojiridhisha hakuna tena tatizo.

Alisema wagonjwa wanaofika kituoni hapo ni wale ambao waliwarejesha baada ya hali zao kuwa nzuri, lakini wakarejea tena baada kujisikia kama wanaumwa na koo.

“Wagonjwa zaidi wanaokuja ni wale tuliowarejesha mwanzo nyumbani, wakisema wanapata maumivu kwenye koo. Wanapatiwa matibabu na kurejea kwao,” alisema Bw Ali.

Hata hivyo, Bw Ali alisema Serikali ya wilaya hiyo inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kutoogopa, huku akihimiza yeyote aliye na dalili akimbilie kituoni hapo.