Makala

Jinsi Rudisha aliacha kutimka akageuka balozi wa mazingira

June 3rd, 2024 3 min read

NA ELIAS MAKORI

MARA ya mwisho David Rudisha alivuma katika mataifa ya Uswizi, Norway, Sweden, na Denmark ilikuwa wakati aliibuka na kuvunja rekodi za riadha.

Mitimko yake kule Sweden ndiyo ilimwinua kutoka kuwa bingwa chipukizi hadi kiwango cha juu cha kunakili rekodi za dunia.

Rudisha alitawala mbio za mita 800 huko Weltklasse Zurich pamoja na Athletissima Lausanne akitifua vumbi Switzerland.

Na kabla ya hapo, alitamba katika mashindano ya Malmo MAI Galan, nchini Sweden.

David Rudisha alipokuwa anatawala mbio za mita 800. Picha|Maktaba

Wakati huo, alikuwa amekata utepe kwa dakika moja na sekunde 45 kabla ya kuimarisha hadi dakika moja na sekunde 40.

Hii ilikuwa rekodi ya dunia katika mbio za Olimpiki za London ambayo ilitajwa bora zaidi na Rais wa Kamati Andalizi Seb Coe wakati huo.

Baadaye Rudisha alitetea taji lake la Olimpiki jijini Rio De Janeiro, Brazil kabla ya kustaafu mapema sababu ya msururu wa majeraha.

Alistaafu miaka minne baadaye na kujishughulisha na kazi yake ya kawaida ya afisa wa usalama.

Kando na kuwa polisi, nguli huyu amechukua jukumu la ubalozi wa mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa.

Harakati hizi zimemrudisha Uswizi na Uswidi katika siku chache zilizopita; maeneo ambayo anayafahamu fika.

Juma lililopita jijini Geneva, Rudisha alihudhudhuria Bunge la 77 la Shirika la Afya Duniani (WHO) ambapo alitambuliwa kwa upekee na Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus.

“Katika Tuzo ya Mkurugenzi Mkuu wa Mabingwa wa Afya 2024 tunamtambua Rudisha kwa “uongozi wake bora na hatua katika kukuza afya ya jamii na kuhamasisha watu dhidi  ya uchafuzi wa hewa,” alinukuu Dkt Tedros.

Mkuu wa WHO pia alimshukuru Rudisha kwa kushiriki toleo la tano la mpango wa “Walk the Talk: Health for All Challenge.”

Toleo hili kadhalika lilihudhudhuriwa na Waziri wa Afya Susan Nakhumicha, Balozi wa Kenya Geneva Fouzia Abbas, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Afya Dkt Patrick Amoth, na Rais wa Shirikisho la Riadha nchini Jackson Tuwei, ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Riadha Duniani.

Viongozi wengine katika mkutano huo wa Geneva walikuwa pamoja na Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) Thomas Bach na Mchezaji nyota mara sita wa Ligi ya Mpira wa Vikapu Amerika Kaskazini (NBA) Pau Gasol.

Gasol alichezea timu za Memphis Grizzlies, LA Lakers, Chicago Bulls, San Antonio Spurs na Milwaukee Bucks katika kilele cha taaluma yake ya NBA.

Si hao tu, pia alikuwepo Susannah Rodgers, nyota wa Olimpiki ya Walemavu wa Uingereza na mshindi wa medali 17 za dhahabu.

Kwa sasa, Susannah ni mtetezi wa kuhakikisha ushirikishwaji wa watu wenye mahitaji maalum katika nyanja mbalimbali.

Tangu kustaafu kwake, Rudisha amejishughulisha na juhudi za Shirikisho la Riadha nchini na Duniani kukabili athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Mabadiliko ya hali ya hewa yanavyoathiri michezo

Akizungumza na Taifa Leo, gwiji huyu alirejelea safari yake ya riadha na jinsi amekumbatia jukumu lake jipya la kuhifadhi mazingira.

“Mabadiliko ya tabianchi yanaathiri kila mtu duniani na madhara yanaonekana – sote tunaathiriwa kwa njia moja au nyingine,” alisema akiwa Stockholm.

“Umeona mafuriko ya hivi majuzi nchini Kenya na pia katika Michezo ya Olimpiki ya Tokyo ambapo ilibidi mbio za marathon zihamishwe kutoka Tokyo hadi Sapporo kwa sababu hali ya Tokyo ilikuwa ya joto isiyo ya kawaida,” alielezea.

“Mabadiliko ya hali ya hewa yanaathiri michezo na tunapaswa kufanya jambo,” aliongeza Rudisha ambaye alianza riadha akisaidiwa na Mmishonari wa Ireland, Ndugu Colm O’Connel, akiwa katika Shule ya Sekondari ya St Francis Kimuron, kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Akiwa katika shule ya upili, alishiriki mbio za chipukizi akisafiri kwa ndege hadi Malmo mnamo 2007 na kushinda mbio za mita 800 kwenye mashindano ya Malmo MAI Galan kwa kutimka kwa dakika 1:45.10.

Lilikuwa shindano lake la kwanza la kimataifa baada ya kushinda taji la Mashindano ya Dunia ya Vijana (akikimbia kwa dakika 1:47.40) katika Kituo cha Michezo cha Chaoyang huko Beijing mnamo 2006.

 “Kurudi Uswidi kunahusisha kumbukumbu ya kwanza Ulaya nikiwa bado shuleni katika mashindano ya Malmo. Baada ya haya, nilitambulishwa kwenye majukwaa makubwa kama Athletissima Lausanne,” alirejelea.

“Kurudi hapa (Sweden) katika wadhifa tofauti ni jambo la kufurahisha kwa sababu ni mchezo ulionijenga na lazima pia mimi nistawishe michezo.”

Rudisha anatilia mkazo kuwa akilinganisha siku zake huko Iten na nyakati za sasa, athari za ongezeko la joto duniani ni dhahiri katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

“Nyakati hizo, Iten ilikuwa baridi sana na tulihisi hali hii katika mazoezi. Lakini siku hizi, unaweza kutembea Iten asubuhi ukiwa na nguo nyepesi….hiyo si nzuri kwa michezo na inaonyesha ni kweli kuna ongezeko la joto duniani. Kwa hivyo, tunapaswa kufanya jambo kuhusu hilo kwa ajili ya upendo wetu kwa michezo,” alisema

Katika kongamano la Geneva, Shirikisho la Riadha nchini (AK) na Chama cha Riadha cha Uswidi kilitangaza mpango mpya wa kuimarisha ushirikiano wao kuimarisha uendelevu na kuangazia mabadiliko ya hali ya hewa katika riadha.

Imetafsiriwa na LABAAN SHABAAN