Jinsi Taa Steriliser inavyoweza kufanya pesa, vifaatiba na vifaa vya urembo kuwa salama kipindi hiki cha janga la Covid-19

Jinsi Taa Steriliser inavyoweza kufanya pesa, vifaatiba na vifaa vya urembo kuwa salama kipindi hiki cha janga la Covid-19

Na MAGDALENE WANJA

WAKATI visa vya Covid-19 vilianza kuthibitishwa nchini, Phelix Juma na mwenzake Dominic Gachuma walianza kuwaza jinsi ambavyo wangetumia ujuzi wao kupunguza virusi kuenea hasa watu wanaposhika stakabadhi, vifaa na karatasi.

Wawili hao walijuana mnamo mwaka 2015 wakati wa kongamano la Global Entreprenuership Summit ambalo lilihudhuriwa pia na aliyekuwa Rais wa Amerika Barack Obama.

Iliwachukua muda wa miezi mitatu kukamilisha kifaa cha kwanza ambacho kingeweza kusafisha stakabadhi, pesa na hata vifaatiba kuwa salama na kuondokewa virusi vya aina mbalimbali vikiwemo vile vya corona.

“Mnamo mwezi Aprili 2020,visa vingi zaidi vya ugonjwa wa Covid-19 viliendelea kuripotiwa nchini na tuliwaza zaidi jinsi ambavyo tungechangia katika kupunguza maambukizi. Ndipo tukaamua kutengeneza kifaa hicho,” asema Bw Gichuma.

Dominic Gachuma aeleza jinsi Taa Steriliser inavyoweza kutumika. Picha/ Magdalene Wanja

Ilipofikia mwisho wa mwezi Aprili 2020, wawili hao waliikabidhi Mamlaka ya Kudhibiti Nyuklia – Kenya Nuclear Regulatory Authority (KNRA) – kifaa hicho na kufikia Mei 14, 2020, ikawapa majibu na kuwataka wawili hao kuwasilisha matokeo ya majaribio waliokuwa wamefanya.

Phelix Juma (kulia) akiwa na Dominic Gachuma. Picha/ Magdalene Wanja

Iliwachukua muda wa miezi miwili kabla ya kufanya jaribio katika vituo vya utafiti ikiwemo kile cha Chuo Kikuu cha Kenyatta.

“Mnamo Juni 2, 2020, tulikabidhiwa idhini na Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa Nchini (Kebs) pamoja na KNRA ya kutengeneza bidhaa nyingine zaidi ambazo tungeziuza kwa mashirika mbali mbali nchini,” akaongeza.

Walikiita kifaa hicho ‘Taa Steriliser’, jina linalotokana na uwezo wake wa kutumia miale ya mwangaza (ultraviolet rays) kuangamiza viini vya ugonjwa vilivyoko kwenye safu za vitu na vifaa mbalimbali.

Kulingana na Bw Juma, uvumbuzi huu ulitokana na wazo la kwamba watu wengi hujikinga kwa kutumia maji na sabuni kusafisha mikono yao ila baada ya hayo wanashika stakabadhi ambazo hazijasafishwa ziwe salama bila viini.

Juma ana shahada ya somo la Uhandisi wa Kielektroniki aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.

“Niliutumia ujuzi huo katika kuhakikisha kwamba kifaa hicho kimefikia kiwango cha kimataifa,” akasema Juma.

Ili kukamilisha kifaa cha kwanza, wawili hao walitumia Sh200,000.

Kinaweza kutumika katika ofisi au benki kusafisha noti za pesa.

Ili kusafisha stakadhi, kifaa hicho kina sehemu kama vile kabati ambapo hufunguliwa na baada ya kuziweka stakabadhi, mlango hufungwa na kisha kuwashwa kwa kubonyeza kitufe.

Kifaa kimoja kinauzwa kwa bei ya Sh17,000.

Wawili hao waliongeza kuwa wana uwezo wa kutengeneza vifaa zaidi iwapo watapata ufadhili kutoka kwa serikali.

You can share this post!

Kang’ata amtaka Matiang’i arekebishe notisi...

Serikali ya Mwangi Wa Iria yatamatisha utoaji wa kilo...