Makala

Jinsi tumbiri wanavyofanya uharibifu shambani, kuiba pombe

March 1st, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

IKIWA kuna mnyama ambaye amesumbua wakulima wa Murang’a kwa muda sasa, ni tumbiri.

Tumbiri wamezidisha utukutu wao kiasi kwamba kando na kutisha kubaka wanawake, wameingilia tabia za kunyonya ng’ombe,mbuzi na hata nguruwe kunywa maziwa yao.

“Hii si hali tena. Walianza kwa kuharibu mimea na mavuno shambani. Sasa wameingilia tabia za kuingia katika vizimba au nyumba za kuku na kutoa mayai, kuua vifaranga pamoja na kunyonya mifugo ya maziwa katika maboma yetu,” akalia Bi Esther Wangithi kutoka kijiji cha Gaturi.

Alilalama kwamba ngombe wake mmoja yuko na chuchu tatu baada ile ya nne kung’atwa na tumbiri aliyekuwa akimnyonya maziwa.

Bi Wangithi alilia kwamba kero hilo kwa sasa limekuweko kwa miaka 14 “lakini kwa miaka miwili iliyopita mambo yamezidi na nikiamua kumenyana nao wananisongea kwa nia ya kunibaka”.

Alisema wakulima wenzake wamekuwa wakiandika barua kwa shirika la huduma kwa Wanyama Pori (KWS) na pia kwa serikali ya Kaunti lakini hakuna afueni ambayo wamepata.

Bi Christina Mutulu alielezea jinsi tumbiri walivyovamia shamba lake katika Kaunti ndogo ya Ithanga na wakaharibu machungwa yake yote.

Bi Christina Mutulu aonyesha uharibifu wa machungwa katika shamba lake la michungwa katika kijiji cha Junction kilichoko Kaunti ya Murang’a. PICHA | MWANGI MUIRURI

“Ni aibu kwamba tunasemwa kuwa Kaunti ya kilimo lakini juhudi zetu zote zinaelekea kulisha tumbiri. Cha kukera zaidi ni kwamba serikali zote za hapa zinajua kuhusu kero hii lakini hazishughuliki,” akasema Bi Mutulu.

Bw Joseph Ndambuki alisema kuwa maadui wa mkulima wa Murang’a kwa sasa ni ukame, ukosefu wa soko, madalali na tumbiri waharibifu.

“Hao tumbiri ni kero kwelikweli. Cha kushangaza ni kwamba ukiwavamia na uue mmoja tu, utaona kamanda wa polisi langoni pako akitaka kukuweka pingu kwa msingi wa kuvamia kivutio cha utalii,” akasema Bw Ndambuki.

Bw Joseph Ndambuki akiwa shambani mwake. Alilia kwamba uharibifu wa tumbiri shambani mwake umesababisha hasara kubwa. PICHA | MWANGI MUIRURI

Alilalama kwamba “serikali hutoa taswira kwamba wanyama ndio wa hadhi zaidi katika maisha kuliko binadamu”.

Aliteta kwamba “ni kama serikali ingependa kufanya kazi na wanyama mashinani kwa kuwa hawalalamiki ukosefu wa madawa hospitalini na ufisadi wa mbolea ya ruzuku kama binadamu”.

Bw Charles Kimani alisema kwamba tumbili wamevamia maeneo ya Ithanga/Kakuzi kwa kiwango kikuu.

“Hata nasikia wapishi wa pombe haramu kando ya mito ya hapa wanalalamika kwamba siku hizi tumbiri hao wanahepa na vibuyu vya pombe,” akasema Bw Kimani.

Aliongeza kwamba wakati tumbiri hao wamevamia pombe hiyo na kuibugia, ile kelele ya kilio na kicheko ambayo hutanda mashambani mwetu kutoka kwao huwa ni ya ajabu.

Alisema eneo la Ithanga linaweza likajitosheleza kwa chakula cha lishe na cha biashara “lakini hali ilivyo kwa sasa haiwezekani kwa kuwa wanyama hawa hawatupei mwanya wa kushirikisha kilimo”.

Aliyekuwa Waziri wa Kilimo wa Kaunti ya Murang’a Albert Kimathi alisema kwamba shida hiyo inafaa kulaumiwa wabunge wa eneo hilo.

“Udhibiti wa wanyamapori pamoja na Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS) ni jukumu la serikali kuu. Ina maana kwamba wabunge kama nyapara wa serikali kuu ndio wanafaa kuwajibishwa mzigo wa kusaka suluhu la wanyama hao,” akasema Bw Kimathi.

Aliongeza kwamba kilimo nacho kikiwa ni jukumu la serikali ya kaunti, utawala wa Gavana Irungu Kang’ata unafaa kuweka presha kwa serikali kuu itume maafisa wa KWS kwa nia ya kutokomeza wanyama hao.

Afisa mkuu wa KWS katika Kaunti ya Murang’a Bw Laurence Kariuki alisema kwamba wakulima hao wanalia kilio cha haki.

“Tunajua kwamba kuna shida kubwa eneo hili na ndiyo sababu tumesajili maafisa 97 wa kutusaidia kupambana na kero la wanyama eneo hili. Mwaka wa 2015 tulikuwa na tumbiri takribani 35,000 lakini hadi sasa wanaweza kuwa wamezaana hadi kufikia 200,000,” akasema.

Seneta wa Murang’a alisema idadi hiyo ya tumbili ni ya juu kiasi kwamba “wangekuwa wapiga kura wangetengewa nyadhifa kadha katika serikali ya Kaunti”.

Alisema anakubaliana na wenyeji kwamba wanyama hao ni adui wa kimaendeleo ma wanafaa kukabiliwa kwa njia yoyote ile ili watokomee.

“Ukikadiria uharibifu wa wanyama hao, ikiwa kila mmoja ataharibu utajiri wa Sh5 tu kwa siku, ina maana kwamba kila siku Kaunti ya Murang’a inapoteza zaidi ya Sh1 milioni, zaidi ya Sh30 milioni kwa mwezi na Sh365 milioni kwa mwaka,” akasema.

Bw Nyutu alisema kwamba “wabunge wanafaa waunde sheria  za kulipa waathiriwa fidia huku nayo serikali ya Kaunti ikihitajika kushirikiana na ile kuu kusaka afueni kwa wakulima wetu”.

Bw Nyutu alisema kwamba tumbiri hao wangegeuzwa mifugo, kila watu watu watano wa Kaunti wangemiliki mmoja “na jinsi muda unavyosonga, huenda idadi ya tumbiri izidi ya wakazi kabla ya 2040”.

Mwaka wa 2018 gavana wa wakati huo Mwangi wa Iria alisajili baadhi ya makundi yawinde tumbiri hao lakini mpango huo ukasambaratika baada yake kukosa kuwalipa kama walivyokubaliana.

Wengine nao walitumia mitego ambayo serikali hiyo iliwapa kunasa tumbiri hao na kisha kuwageuza kuwa mlo hali ambayo ilifanya KWS kulalama ikisema huo ulikuwa uwindaji haramu.

[email protected]