Michezo

Jinsi ufadhili wa Mombasa Maize Millers unavyofanikisha Taifa Ngano Super Cup

May 24th, 2020 2 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

UKOSEFU wa udhamini umekuwa sababu kubwa ya kuzorota kwa soka Pwani na kidonda ambacho klabu na viongozi wa soka wamejaribu kukiponesha bila ya mafanikio.

Kampuni ya Mombasa Maize Millers Limited imekuwa ikijitolea kila mwaka kudhamini mashindano ya Unga yaani Taifa Ngano Super Cup yanayotayarishwa na kuchezwa kwenye uwanja wa Mombasa Sports Club (MSC).

Mbali na mashindano hayo, kampuni hiyo pia imekuwa ikitoa kitita cha pesa na zawadi muruwa kwa timu zinazofanya vizuri kwenye mashindano hayo mbali na kushirikiana na tawi la Pwani Kusini la Shirikisho la Kandanda Nchini (FKF) kuandaa mashindano kama hayo Kwale.

Mkurugenzi wa Mombasa Maize Millers, Ali Ahmed Ali Bashammah (wa nne kulia) akikabidhi hundi ya udhamini wa mashindano ya Taifa Ngano Super Cup kwa maafisa wa FKF Pwani Kusini. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Mwenyekiti wa FKF Pwani Kusini, Gabriel Mghendi amesema wana mpango wa kukutana na wakuu wa kampuni hiyo ya Mombasa Maize Millers kuhusiana na mashindano ya mwaka 2020 ya Kaunti ya Kwale.

“Kampuni hiyo imekuwa ikisaidia pakubwa maendeleo ya soka katika kaunti za Kwale na Mombasa kwa kudhamini mashindano ambayo yamekuwa maarufu kufanyika kila mwaka katika kaunti hizo mbili za jimbo la Pwani.

“Nina matumaini makubwa itaendelea kudhamini mashindano hayo ambayo yanarudisha mashabiki wengi viwanjani. Tunaamini kampuni itaendelea kudhamini ili kutimiza lengo lake la kuwatoa vijana mitaani ambapo wanajihusisha na maovu,” akasema Mghendi.

Mghendi alisifu kampuni hiyo kwa udhamini wao wa mashindano hayo pamoja na mashindano mengine wanayodhamini eneo la Pwani na akaitaka iendelee kudhamini michezo kwa ajili ya kuwafanya vijana kuinua vipaji vyao.

“Udhamini wao umesaidia pakubwa kuinua hali ya soka Pwani na hata kuna wachezaji wanaochezea timu ya taifa ya Harambee Stars na klabu mashuhuri za hapa nchini, ambapo huchezea timu zao za mitaani na hivyo kuvutia mashabiki,” akasema.

Alimshukuru mno Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Ali Ahmed Ali ambaye alijitolea kwa hali na mali kuhakikisha kampuni hiyo inajitolea kutoa kitita kikubwa cha zawadi kuvutia vijana kucheza soka badala ya kuwaacha wakiwa mitaani bila ya kuwa na la kufanya.

Mghendi amewaomba wachezaji pamoja na maafisa wa klabu wajitulize majumbani na kujikinga ili waepuke madhara ya corona.

“Ninaamini wanasoka wote wanafuata maagizo kutoka klabu zao na nina matumaini ugonjwa huo utatoweka hivi karibuni na soka litarudi uwanjani,” akasema.

Kinara huyo wa FKF Pwani Kusini alisema baada ya janga hilo kutoweka, watakutana na wakuu wa kampuni ya Mombasa Maize Millers kujadili mambo kadhaa na ana matumaini makubwa watadhamini tena ili kuwafurahisha vijana baada ya kuumia bila ya kucheza kwa muda mrefu.

Alitoa wito kwa kampuni zingine ziige mfano wa Mombasa Maize Millers kwa kudhamini mashindano ya soka ya wanaume na wanawake ili wavulana na wasichana wapate kuinua vipaji vya uchezaji wao na wapate fursa ya kuangaziwa na kusajiliwa na klabu kubwa nchini.

“Nina imani kubwa kama mashindano ya mara kwa mara yatakuwa yakifanyika kote mkoani, Pwani itaweza kuwika kwenye mashindano ya kitaifa. Nawaomba wakuu wa kampuni zingine wajitolee pia kudhamini ligi za kaunti na za eneo pana la Pwani,” akasema Mghendi.

Gabriel Mghendi, Mwenyekiti wa FJKF Pwani Kusini. Picha/Abdulrahman Sheriff

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Ali Ahmed Ali Bashammah alisema wanashirikiana na waandalizi wa mashindano hayo kwa ajili ya kuwapa fursa vijana kuinua vipaji vya uchezaji wao.

“Tunafahamu wajibu wetu kwa jamii na ndio maana tunajitolea kusaidia na kudhamini mashindano yetu ili wapate kucheza mpira na kuacha kujihusisha na maovu yakiwemo yale ya utumizi wa dawa za kulevya na kujihusisha na visa vya uhalifu,” akasema Bashammah.

Baadhi ya mashabiki wa soka wa jimbo la Pwani wa Kaunti nyingine wameomba kampuni hiyo idhamini mashindano ya kila mwaka ili vijana wa sehemu wapate kuonekana ili wapate klabu kuwasajili.