Makala

Jinsi ufugaji wa samaki unavyoweza kusaidia kuimarisha uchumi na kubuni ajira serikali ikiupiga jeki

December 12th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

MBALI na kuwa mkulima hodari wa matufaha, Peter Wambugu pia ni mfugaji wa samaki kwenye dimbwi eneo la Ngobit, Kaunti ya Laikipia.

Wambugu ni mtafiti wa aina yake katika uzalishaji wa matufaha, shughuli aliyoanza miaka ya themanini, mkondo ambao sasa anauelekeza katika ufugaji wa samaki.

Hata ingawa hajakuwa kwenye kilimo cha samaki kwa muda mrefu, Wambugu anakiri kuwa wanyama hao wa majini wana mapato ya kuridhisha.

Ni ufugaji ambao anahisi ukikumbatiwa, utasaidia kuangazia kero la ukosefu wa ajira, hasa miongoni mwa vijana, ila hamasisho ndilo halipo.

“Kikwazo kilichopo ni ukosefu wa hamasisho kwa umma, kuingilia shughuli bora za kilimo kama vile ufugaji wa samaki. Isitoshe, wenye nia hawana fedha, mtaji ili kung’oa nanga,” Wambugu anaelezea.

Maandalizi ya dimbwi au bwawa, ndiyo gharama.

Kulingana na Mhandisi Joseph Oloo, ambaye ni mfugaji wa ng’ombe wa kisasa wa maziwa na pia samaki Kaunti ya Homa Bay, dimbwi la mita 20 kwa mita 25 halipungui Sh100, 000 kulichimba na kuliandaa liafiki vigezo faafu kufanikisha kilimo cha samaki.

“Kazi na gharama huwa katika maandalizi ya eneo la kufugia samaki. Nina mabwawa matano, ambayo kima cha zaidi ya shilingi nusu milioni hakikusalia. Vijana wenye ari kufuga samaki wakipigwa jeki, kwa kuchimbiwa vidimbwi au mabwawa wataweza kujiendeleza kimaisha,” Mhandisi Oloo anadokeza.

Mfugaji huyo hata hivyo, anasema kufuatia kuimarika kwa teknolojia, kuna vidimbwi tamba vinavyotengenezwa kwa mbao na pia mabati, kisha vinaezekwa kwa karatasi ngumu za nailoni, ambavyo anahoji ni vya gharama nafuu.

Tatizo la upungufu wa samaki nchini limaweza kuangaziwa ikiwa serikali kuu kwa ushirikiano na serikali za kaunti zitafanya hamasisho la kutosha kuhusu ufugaji wao na pia kupiga jeki wakulima. Picha/ Sammy Waweru

Anaelezea kwamba dimbwi lenye ukubwa wa mita 20 kwa mita 25, linasitiri kati ya samaki 2, 000 – 2, 500, aina ya Tilapia.

Aidha, Mhandisi Oloo alianza kwa vidimbwi na mabwawa mawili, na kufikia sasa ana matano.

“Samaki wa bei ya chini ni Sh100 katika mradi wangu. Hii ina maana kuwa sikosi kuweka kibindoni zaidi ya Sh200, 000 wanapokamaa. Nikiondoa gharama ya matumizi; ndiyo lishe, leba na mahitaji mengine yanayoibuka, ninasalia na mapato ya kuridhisha,” anafafanua mkulima huyo, akihimiza serikali kutilia mkazo kilimo cha samaki.

Anasema, gharama ya lishe ya samaki ni ya chini ikilinganishwa na ufugaji mwingine, ikizingatiwa kuwa hawahitaji ulinzi endapo mazingira ya wanamofugiwa ni salama.

Samaki ni kati ya wanyama wanaosifiwa kuwa na nyama tamu nyeupe na yenye ladha, isiyo na chembechembe za Cholesterol.

Uhaba wa samaki nchini ni bayana kutokana na bei ya juu ya bidhaa hiyo sokoni. “Kipindi hiki cha Covid-19 bei ya samaki imepanda kwa kasi,” anasema Mourine Ombiri, mfanyabiashara wa samaki kiungani mwa jiji la Nairobi.

Ni gapu ambayo ikiangaziwa itasaidia kutatua upungufu wa samaki nchini, hatua ambayo pia itachangia kubuni nafasi za ajira.

Vile vile, ufugaji wa samaki nchini ukikumbatiwa na kuimarika, utakuwa miongoni mwa shughuli za kilimo na ufugaji zinazovunia serikali ushuru.

Serikali ya Kaunti ya Nyeri, chini ya Gavana wake Mutahi Kahiga, katika siku za hivi punde imeonekana kuzindua miradi mbalimbali ya ufugaji wa samaki. Nyayo hizo pia zimefuatwa na Kaunti ya Makueni.