Jinsi Uhuru alivyosaidia Ruto kuchaguliwa rais wa 5

Jinsi Uhuru alivyosaidia Ruto kuchaguliwa rais wa 5

NA BENSON MATHEKA

MKONO wa Rais Uhuru Kenyatta ulikuwa dhahiri katika uchaguzi wa mwaka huu huku akimpigia debe mgombea urais wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga na kumpinga vikali William Ruto wa muungano wa Kenya Kwanza.

Mara kwa mara, Rais Kenyatta aliwarai wapigakura kumchagua Bw Odinga akisema ndiye ataendeleza miradi na ajenda zake.

Msimamo wake ulionekana kumjenga Dkt Ruto hasa eneo la Mlima Kenya ambako alizoa kura nyingi.

Ni Rais Kenyatta aliyeleta pamoja vyama zaidi ya 26 chini ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kumsaidia Bw Odinga kumkabili Dkt Ruto ambaye alianza kujipigia debe miaka minne na nusu kabla ya Agosti 9.

Vile vile, ni handisheki ya Rais Kenyatta na Bw Odinga mwaka wa 2018 iliyomfanya Dkt Ruto kuanza kampeni za mapema ingawa Rais Kenyatta alimlaumu kwa kumkaidi na kuendeleza siasa badala ya kutekeleza ajenda ya Jubilee.

Dkt Ruto aliyetengwa serikalini katika muhula wa pili wa Jubilee alijijengea umaarufu katika ngome ya Rais Kenyatta ya Mlima Kenya akimtaja kiongozi wa nchi kama aliyesaliti wakazi kwa kukumbatia mpinzani wake mkuu kwenye uchaguzi wa 2017.

Kutengwa kwake serikalini na katika chama tawala cha Jubilee kulimfanya Dkt Ruto kuzidisha uasi na kubuni chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambacho alitumia kupenya katika eneo la Mlima Kenya na kupata umaarufu kuliko Rais Kenyatta, ilivyodhihirika katika matokeo ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Wakazi wa Mlima Kenya walimkumbatia wakisema wanafaa kurudisha mkono kwa kumuunga Rais Kenyatta kwa miaka kumi tangu 2013 walipochaguliwa kuongoza kwa muhula wa kwanza.

Kulingana na mdadisi wa siasa Dkt Isaac Gichuki, hatua ya Rais Kenyatta kumtenga Dkt Ruto ilimjenga zaidi katika eneo la Mlima Kenya na kumwezesha kupata kura nyingi zaidi eneo hilo.

“Kwa kila hali, mkono wa Rais Kenyatta ulichangia matokeo ya kura ya urais kwenye uchaguzi wa mwaka huu kwa vile alikuwa akimpendelea Bw Odinga kuwa mrithi wake. Pia, Dkt Ruto alitumia hatua hiyo kujipigia debe eneo la Mlimani na matokeo yanaonyesha alivuna pakubwa,” asema Dkt Gichuki.

Anasema kwamba kama Rais Kenyatta hangehusika moja kwa moja na siasa za urithi wake pengine matokeo yangekuwa tofauti.

“Alimkweza Bw Odinga Mlima Kenya na pia kwa kumsaidia kuunda muungano wa Azimio la Umoja One Kenya ambao alishawishi vyama zaidi ya 26 kumuunga kiongozi huyo wa ODM. Rais Kenyatta pia alihakikisha maafisa wa serikali wakiwemo mawaziri na makatibu wa wizara walimpigia debe Bw Odinga. Tuliwaona katika mikutano ya kampeni wakitangaza misimamo yao hadharani,” alisema.

Dkt Ruto alikuwa akilalamika kuwa maafisa wa serikali wakiwemo mawaziri, maafisa wa utawala na usalama walitumiwa kumsaidia Bw Odinga.

  • Tags

You can share this post!

Ruto abwaga Raila kuwa rais wa tano wa Kenya

IEBC yachapisha rasmi kwa gazeti la serikali Ruto ndiye...

T L