Jinsi vijana, wanamuziki walivyopiga kampeni za Azimio eneo la Mlima Kenya mnamo Jumamosi

Jinsi vijana, wanamuziki walivyopiga kampeni za Azimio eneo la Mlima Kenya mnamo Jumamosi

NA LAWRENCE ONGARO

VIJANA kutoka kaunti za Kiambu na Murang’a, walijitokeza wazi kuendesha kampeni za kumvumisha mgombea urais wa Azimio La Umoja-one Kenya Raila Odinga debe.

Vijana hao walioandamana na wanamuziki tofauti kutoka Mlima Kenya waliahidi kuwa watawabeba wagonjwa na wakongwe hadi kwenye vituo vya kupigia kura ili Odinga na mgombea mwenza Martha Karua, waweze kupata kura nyingi kutoka Mlima Kenya.

Vijana hao walikuwa chini ya kikundi kinachojiita Kiambu, Murang’a Youth Forum.

Walisema watafanya juhudi kuona ya kwamba wanapenya kona zote ili kuwarai wananchi wapigie Odinga kura bila kusita.

Vijana hao wakiongozwa na Bw Joseph ‘Monjos’ Kamau, walisema ajenda yao kuu itakuwa kuingia kila boma katika maeneo hayo mawili kuona ya kwamba muungano wa Azimio unaunda serikali itakayochukua baada ya Rais Uhuru Kenyatta kustaafu.

“Uchunguzi wetu unatujulisha kuwa majina ya Raila Odinga na Martha Karua yamesambaa kama moto katika eneo zima la Mlima Kenya ambapo hata mkongwe kijijini anatambua viongozi hao wawili,” alifafanua kinara huyo wa vijana.

Vijana hao walifanya msafara kwenye malori.

Baadhi ya wanamuziki mashuhuri waliondamana na vijana hao kupigia debe Azimio ni Peter Kigia, Ben Githae, Wa Thuo, Regina Muthoga, na Zachary Wanderi.

Bw Kamau alisema wamekuwa wakifuata mwelekeo uliotolewa na Rais Kenyatta kwa sababu wanaamini ameleta mabadiliko mengi katika miaka kumi ambayo amekuwa uongozini.

“Sisi kama vijana chipukizi hatungekubali kupotoshwa na kiongozi yeyote na kwa hivyo kiongozi wetu mpendwa Kenyatta ametupatia mwelekeo,” alifafanua Bw Kamau.

“Tuna uhakika uongozi wa Odinga na Karua utaimarisha maisha ya Wakenya na kuendeleza miradi yote anayoacha Rais Kenyatta. Kwa hivyo ni vyema kuwa na mwelekeo mmoja wa kijamii,” alijitetea Bw Kamau.

 

Bi Regina Muthoga ambaye ni msanii alisema kuwa wamezunguka eneo la Mlima Kenya karibu miezi minne sasa na waneridhika kuwa wafuasi wengi wameanza kuegemea upande wa muungano wa Azimio chini ya kauli mbiu ya Inawezekana.

  • Tags

You can share this post!

Brighton waangusha Man-Utd ya kocha Ten Hag katika EPL...

WANDERI KAMAU: Wakati wa Kenya kuonyesha imeiva...

T L