Habari Mseto

Jinsi viongozi na watumiaji mitandao ya kijamii wamepokea habari za kifo cha Moi

February 4th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

WATUMIAJI wa mitandao ya kijamii wameelekeza risala za pole kwenye kurasa zao kufuatia kifo cha Mzee Daniel Toroitich Arap Moi ambaye alikuwa Rais wa Pili wa Jamhuri ya Kenya.

Mzee Moi ameaga dunia mapema Jumanne katika Nairobi Hospital.

Chini ya utawala wa Rais huyo mstaafu na ambaye kwa sasa ni marehemu, kati ya mwaka 1978 – 2002, anakumbukwa kwa mengi.

Alichukua hatamu baada ya kifo cha Rais mwanzilishi wa taifa hili, Hayati Mzee Jomo Kenyatta.

Neno ‘Nyayo’ linapotajwa, linahusishwa na Mzee Moi.

Katika sherehe za kitaifa, akiingia uwanjani kwa gari maalum la Amiri Jeshi Mkuu, Rais huyo aliinua na kutikisa kidole cha shahada, huku akikariri ‘Nyayo’, wananchi nao wakiiga hilo. Pia alitumia rungu yake kuongoza kukariri jina hilo.

Kwenye mitandao ya kijamii wachangiaji wamefufua kumbukumbu zao kwa mazuri aliyowafanyia katika enzi yake akiwa Rais wa Jamhuri.

Mtumiaji mtandao wa Facebook, Gedion Mwangi Kabugi amechapisha picha za pakiti za maziwa yaliyoasisiwa na Mzee Moi, na ambayo yalikabidhiwa wanafunzi katika shule zote za msingi na za umma nchini miaka ya tisini.

“Watu wa enzi zetu, tunaweza kumsahau Moi kweli? Haya maziwa tulikuwa tunayanywa sana, kisha tunakata vipande vya pakiti na kucheza karata. Nakumbuka 1993 ilisemekana maziwa hayo yana vidole vya binadamu, tukaanza kuyamwaga ila madai hayo yalikuwa uongo mtupu,” anafafanua mchangiaji huyo.

Kabugi kwenye simulizi yake, anakumbuka wakati baba yake akiwa mwalimu mkuu wa shule ya msingi aliyosomea, alikuwa akiingia ofisini kisiri na kuyanywa maziwa ya Nyayo. “Ningekunywa zaidi ya pakiti tatu. Mungu ailaze roho yake mahali pema Mzee Moi, hatutakusahau,” anaeleza.

Mchangiaji mwingine, Wa Biashara Simon, anasema tangu Rais Moi astaafu, ameyakosa maziwa hayo ya Nyayo.

Susan Mwangi naye anataja marehemu kama kiongozi ambaye aliwapa wanafunzi motisha ya kusoma.

“Hatukuwa tukikosa shuleni kwa sababu ya maziwa,” Susan amemsifu Moi.

Nasrin Naserian anamuomboleza kama kiongozi aliyehubiri utangamano na amani.

“Kama kuna mtu niliyekosea, ninaomba anisemehe,” Nasrin anamkuu Mzee Moi akisema kauli hiyo ni ishara kuwa alikuwa kiongozi aliyethamini amani.

Mwili wa kiongozi huyo umehifadhiwa katika chumba cha Lee Funeral jijini Nairobi, ambapo viongozi na wanasiasa mbalimbali wanaendelea kumiminika kuutazama mwili.

Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula, kwa upande wake amesema alikuwa mmoja wa mawakili wa Mzee Moi.

“Moi aliniteua mnamo 1993 kuingia bungeni. Nilikuwa na fursa ya kipekee kuwa mmoja wa mawakili wake,” akasema Bw Wetang’ula akitoa salamu zake za pole.

Marehemu pia ametajwa kama kiongozi ambaye hakutaka mzaha kazini.

“Alikuwa mcha Mungu na kabla kuanza kazi lazima angesoma Biblia. Alikuwa akiamka alfajiri na mapema kuhudumia taifa,” anasema Franklin Bett ambaye alihudumu chini ya serikali ya Mzee Moi.

Marehemu pia anatajwa kama profesa wa siasa, Bett akisema alielewa bayana mchakato na mikakati ya siasa. Licha ya sifa zake, baadhi walimlaumu kwa utawala wa kidikteta.

Wakati wa usomaji habari, ambapo Voice of Kenya (VoK) kwa sasa ndiyo KBC Radio Taifa, ndicho kilikuwa kituo cha redio cha kipekee, sharti taarifa ya kwanza ingekuwa ya Rais Moi.

Japo inaelezwa alizaliwa 1924 mwandani wake wa karibu Lee Njiru amesema Mzee amefariki akiwa na umri unaozidi miaka 100.

Vilevile Raymond Moi amesema Mzee alikuwa na umri unaozidi miaka hii ya 95 na 96 inayosemwa.