Habari Mseto

Jinsi wabunge wawili walivyojenga shule kipindi cha janga la Covid-19

November 17th, 2020 1 min read

Na WINNIE ATIENO

WABUNGE wawili Kaunti ya Mombasa wametumia kipindi hiki cha janga la Covid-19 kujenga shule na kuboresha miundomsingi na nyenzo muhimu za kufanikisha elimu katika taasisi hizo.

Miezi tisa baada ya kufungwa kwa shule zote nchini, shule kadhaa wilayani Nyali na Changamwe zimepata sura mpya huku madarasa yakiongezwa kushughulikia idadi kubwa ya wanafunzi.

Katika eneo la Changamwe, mbunge Omar Mwinyi amejizatiti kuboresha miundomsingi katika shule zilizoko wilayani mwake wakati huu ambapo taasisi za elimu zimefungwa.

Bw Mwinyi alisema ataendelea kuboresha sekta ya elimu akiwataka wanafunzi kutia bidii masomoni.

Alitaja ujenzi unaoendelea katika shule ya upili ya bweni ya Airport ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 70.

“Awamu ya kwanza ya ujenzi wa shule hiyo inatimia kukamilika baada ya kumalizwa kwa madarasa manne, vyoo, mabweni, maabara na afisi za walimu. Kuwekeza katika sketa ya elimu hususan miundomisingi bora huimarisha elimu bora,” alisema.

Mbunge huyo alisema shule hiyo itashughulikia elimu ya watoto wenye ulemavu.

Bw Mwinyi anajenga shule ya kwanza ya upili ya pekee ya wasichana eneo la Changamwe.

“Tayari bloke ya madarasa matatu yamemalizwa. Ili wanafunzi wetu wapiti mitihani lazima wapatemazingira bora. Shule hiii mpya itaboresha amri ya serikali ya kuhakikisha watoto wote wanaenda shuleni,” alisisitiza.

Naye mwenzake wa Nyali alisema shule zitakapofungiliwa mwakani wanafunzi watapata mazingira bora.

Bw Ali amekamilisha ujenzi wa shule ya msingi na ya upili ya Kwa Bullo.

“Watoto wetu wa wodi ya Kadzandani watasoma bure. Ujenzi wa shule ya wasichana ya Mohamed Ali unaendelea,” alisisitiza.

Wawili hao ndio wabunge ambao wametilia mkazo sekta ya elimu.