Habari Mseto

Jinsi Wakenya walivyofika Pirates kutamatisha msimu wa sherehe

January 4th, 2024 1 min read

NA CHARLES ONGADI

MNAMO Jumanne wiki hii, siku moja tu baada ya sherehe za Mwaka Mpya kupamba moto na kufika kilele, raia walimwagika maeneo tofauti Pwani.

Wananchi walimiminika katika ufuo wa Jomo Kenyatta Public Beach amaarufu kama ‘Pirates Beach’ kuondoa maruerue.

Vijana na watoto walionekana wakiogelea baharini kwa furaha.

Kulingana na Bw Gabriel Kamau ambaye alifika Mombasa akitoka jijini Nakuru, likizo ya wiki moja akiwa na familia yake ilimpa nafasi nzuri ya kupunga upepo.

“Mombasa kuna joto na kwa sasa nimeshindwa kukaa hotelini ndiposa nikaamua kuleta familia hapa kufurahia upepo mwanana,” akasema Bw Kamau.

Naye Bw Calvin Opande kutoka mtaa wa Bangladesh katika eneobunge la Jomvu, Mombasa, anafichua kwamba alikaribisha mwaka mpya akiwa katika bustani ya Mama Ngina Waterfront, Likoni kwa burudani aali usiku kucha na Januari 2, 2024, ilipofika, akaamua kufika Pirates kufunga sherehe hizo.

Baadhi ya wananchi walionekana wakijivinjari kandokando mwa ufuo wakifurahia mandhari wakati baadhi wakiogelea maji ya karibu.

Uchunguzi wa Taifa Leo ulibaini kwamba wananchi wengi waliofika hapa hawakuonekana na haraka ya kutaka kuogelea bali walionekana kufurahia tu siku za mwisho mwisho za sherehe za Mwaka Mpya.

Kwa upande mwingine, wafanyabiashara katika eneo hilo waliendelea kuvuna kama kawaida kutoka kwa wateja walioendelea kufika hapo.

Madafu yakiuzwa kwa wateja Pirates Beach wakati wengi walifika hapo kuondoa maruerue ya ukweli kwamba msimu wa sherehe ulikuwa unafika tamati. PICHA | CHARLES ONGADI

Kulingana na Bw Athumani Bakari anayekodisha viti katika ufuo huo, anakiri biashara ilinoga zaidi mkesha wa mwaka mpya ambapo watu kweli walijitokeza kwa wingi.

Bw Edward Ngao ambaye hufanya kazi katika kikosi cha waokoaji katika ufuo huo, alisema tangia sherehe za Krismasi hadi kufika Mwaka Mpya hakujaripotiwa visa vyovyote vya mtu kuzama majini.