Makala

Jinsi wanafunzi wa chuo walivyong’ang’ania Githeri Rasta bila malipo

April 8th, 2024 1 min read

NA LABAAN SHABAAN

WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Kenyatta na wakazi wa mtaa wa kibiashara wa KM walimimika hotelini kufurahia kande maarufu maarufu Githeri Rasta.

Kande ni mchanganyiko wa mahindi na maharagwe, uliopikwa.

Kilichofanya foleni hotelini kuwa kubwa ni hali kuwa mwanabiashara mbunifu wa chakula hicho alitoa chamcha bila malipo.

“Baada ya kuona tunapewa chakula bure imebidi nije sababu hata muhula wa chuo umeisha na pesa zangu zimeisha,” alifurahi mwanafunzi aliyejitambulisha kwa jina Dancun Mandi.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) wapanga foleni kuchangamkia githeri rasta. PICHA | LABAAN SHABAAN

“Sikuwa najua githeri rasta ni nini na kwa hivyo imebidi nije nijionee mwenyewe,” alikiri mwingine aliyekuwa ameduwaa kuhusu uvumbuzi huu wa mapochopocho.

Haya yanajiri baada ya mlo huo kutamba mtandaoni Januari 2024 – mwezi unaoaminiwa kuwa ‘wa njaa.’

Chakula hiki, githeri rasta, ni mseto wa tambi, mahindi na maharagwe.

Mamia ya wanafunzi walifika katika Dha Lakers Dishes kuonja, kujua na kula bila malipo.

Lango la mkahawa wa Lakers Dishes ambao umekuwa maarufu kwa ubunifu wa chakula. PICHA | LABAAN SHABAAN

Meneja wa hoteli hiyo Lenson Munene ameondokea kuwa gumzo mitandaoni kwa kubuni vyakula ainati.

Soma Watu ni kupambana na ‘githeri rasta’ Januari – Taifa Leo (nation.co.ke)

“Nilianza kujulikana kwa ‘ugali pambana’ na baadaye githeri rasta ikanifanya maarufu sana nchini na hata nchi za ughaibuni,” alikumbuka Lenson.

Kila msimu wanabiashara wa mikahawa huibuka na mbinu nyingi za kuandaa mapochopocho nafuu kwa wanachuo wanaotafuta chakula bora kisicho ghali.

Mwanabiashara mbunifu wa vyakula Lenson Munene. PICHA | LABAAN SHABAAN

“Ili ubaki katika soko kwa kuwa na wateja wengi lazima uwe mbunifu zaidi ya washindani wako. Hii ndiyo sababu mimi hujikuna kichwa kila siku kubuni mitindo ya chakula,” alifunguka Munene.

Soma Ugali Pambana: Wanachuo sasa wala ugali kwa harufu ya nyama kupambana na hali ngumu ya maisha – Taifa Leo (nation.co.ke)

Wateja walikiri kuwa tambi hizi huongeza ladha kwenye pure (githeri) na kuifanya tamu kwa mionjo ya nyama ya kuku ama ng’ombe.

Msimamizi wa Mauzo katika Kampuni ya tambi za Indomie Lucy Nyambura Maina alishirikiana na mikahawa tofauti kuhakikisha wateja wanafurahia chakula hicho maarufu.