Jinsi wanaume wanavyoporwa mali kwa ahadi za ngono

Jinsi wanaume wanavyoporwa mali kwa ahadi za ngono

NA MARY WANGARI

VISA vya wahalifu wa-naotumia wanawake kuwahadaa wanaume kupitia mitandao ya kijamii na sehemu za burudani vimeongezeka pakubwa nchini, Taifa Leo imebaini.

Katika kisa cha hivi karibuni, wapelelezi kutoka Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) wanawazuilia washukiwa watano, miongoni mwao wanawake watatu, kwa kumteka nyara mwanamume mmoja kabla ya kumwitisha Sh100,000 ili kumwachilia huru.

Kisa hiki kimejiri siku chache tu baada ya maafisa wa DCI kuwakamata wanachama wa genge hatari la wanawake almaarufu Basmati Babes ambalo limekuwa likiwavizia wanaume kwenye vilabu kwa kuwatilia ‘mchele’ na kisha kuwaibia.

Uhalifu huo sasa umechukua mkondo mpya ambapo wanawake wanatumiwa kuwapumbaza wanaume, hasa wa asili ya Kimagharibi, kwa ahadi moto moto za kushiriki uroda kabla ya kuwageuka, DCI imefichua.

“Katika njama iliyopangwa vyema, wanawake watatu waliokamatwa huwavizia wanaume mitandaoni wakiwaahidi burudani murwa na wanaume hao waliovutiwa, hutanguka mtegoni. Huku wakipendelea wanaume wa asili ya Kimagharibi, wanawake hao huwaelekeza wanaume waliopumbazika kwenye nyumba moja nyuma ya Naivas Supermarket, Ruaka, wakiahidi usiku uliojaa ‘miereka’ kutoka kwa wanawake wawili au watatu jinsi anavyopendelea.”

“Lakini kabla ya kuanza ngoma, mlango hubishwa ghafla ambapo mwanamume anayejifanya mpenzi wa mmoja wa wanawake hao hujitokeza na kuvuruga usiku. Kinachofuata ni kuitishwa fidia kwa kutegemea uzito wa mtu,” ikasema DCI.

Mnamo Alhamisi, makachero kutoka kikosi maalum ambao wamekuwa wakifuatilia genge hilo waliwakamata washukiwa hao Joseph Makau Mulatya, Patrick Wekesa Omosa, Rehema Njeri, Vigilance Mumbi na Hadija Ong’ai.

“Katika kisa cha jana, makachero kutoka kikosi maalum ambao wamekuwa wakifuatilia genge la wanawake hao walivamia nyumba ambamo mwanamume alikuwa amezuiliwa walipompata akiwa uchi, huku washukiwa wakisubiri kwa hamu Sh100,000 kutumwa kwa Mpesa ili kumwachilia huru mwanamume huyo. Mhasiriwa alikuwa amewapigia simu jamaa zake akidai amehusika kwenye ajali na anahitaji Sh100,000 za matibabu.”

Maajenti hao walifuata vidokezo vya upelelezi vilivyowaelekeza hadi katika nyumba alimozuiliwa mhasiriwa.

Waliunganisha tukio hilo na kisa kilichotokea mwezi uliopita ambapo mwanamume mmoja aliandamwa katika eneo la Parklands, Nairobi na kuporwa Sh450,000.

Mwanamme huyo amewatambulisha washukiwa waliomwibia pesa zake kutoka kwenye akaunti ya benki kwa kutumia mtindo sawa na huo.

  • Tags

You can share this post!

Liverpool vs Real Madrid: Leo ni leo!

Karua ahofia kura kurudiwa kama 2017

T L