Jinsi ya kuandaa biriani ya nyama ya ng’ombe

Jinsi ya kuandaa biriani ya nyama ya ng’ombe

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 15

Muda wa mapishi: Dakika 50

Walaji: 3

Vinavyohitajika

 • nyama kilo 1
 • kitunguu saumu kilichosagwa pamoja na tangawizi kijiko 1
 • pilipili iliyosagwa kijiko 1
 • bizari iliyosagwa kijiko 1
 • mdalasini kijiko 1
 • maziwa mala vijiko 5
 • pilipili mboga 1 iliyokatwakatwa
 • vitunguu maji 3 vilivyokatwakatwa
 • nyanya 8 zilizosagwa
 • nyanya ya mkebe vijiko 4
 • dania
 • viazi 4 vilivyokatwakatwa
 • mafuta ya kupikia
 • chumvi
 • mchele nusu kilo
 • rangi ya manjano na rangi ya kijani

Maelekezo

Weka nyama kwenye sufuria pamoja na mahitaji yote ya rojo isipokuwa viazi, kitunguu maji, dania na mafuta.

Koroga vizuri, ubandike motoni – mekoni – uache nyama iendelee kuiva. Uunaweza ukatumia pressure cooker ili nyama iive haraka na ilainike vizuri.

Kaanga kitunguu maji mpaka kiwe na rangi ya kahawia kisha kiweke pembeni.

Vikaange viazi kwenye mafuta mpaka viive lakini visiive sana. Viweke pembeni vikishaiva.

Tazama rojo lako na kama nyama imeiva na imekauka, weka viazi na vitunguu ulivyovikaanga na pia dania na mafuta na uliache lichemke kwa dakika tano. Rojo lipo tayari.

Endelea na matayarisho ya wali.

Bandika motoni – mekoni – sufuria ya mchele uliouosha vizuri na ufunike mpaka uanze kuiva kisha mimina maji. Urudishe motoni na utie mafuta.

Tengeneza shimo upande mmoja utie rangi ya manjano na upande mwingine utie rangi ya kijani.

Funika wali wako uendelee kukauka na kuiva vizuri.

Biriani iko tayari.

Andaa mezani na hakikisha una kachumbari na pilipili uliyoikaanga vizuri na ufurahie.

You can share this post!

Waiguru, Ngirici wazidi kuonyeshana ubabe

Wanafunzi 2,000 Mukuru wapigwa jeki kielimu

T L