Jinsi ya kuandaa burger ya nyama ya ng’ombe

Jinsi ya kuandaa burger ya nyama ya ng’ombe

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

Muda wa kuandaa: Dakika 20

Muda wa kupika: Dakika 20

Walaji: 3

Vinavyohitajika

· nyama ya kusaga kilo ½

· mikate mitatu ya burger – baga – (kata katikati kila mkate upate vipande sita)

· siagi kijiko kikubwa

· vijijo viwili vya tomato ketchup

· majani matatu ya lettuce (mboga ya saladi)

· vijiko viwili vikubwa vya mayonnaise

· nyanya moja kubwa kata slice za duara upate tatu

· kitunguu maji kimoja kikubwa kata duara upate slaisi tatu

· slesi tatu za jabini

· mafuta ya kupikia kijiko kimoja

Maelekezo

Chukua nyama ya kusaga mbichi weka katika bakuli, weka chumvi, changanya kisha tengeneza madonge matatu (usiyafanye membamba sana lakini zingatia yawe manene kiasi) yatoshane na mikate ya baga. Ukimaliza chukua kikaangio weka mekoni. Wakati moto ungali wa joto la chini, weka mafuta ya kupikia kijiko kimoja na yakishapata moto kiasi, weka madonge yako ya nyama na uyakaange juu na chini yapate rangi. Yakishakuwa tayari, weka pembeni.

Katika kikaangio kilicho katika meko, weka kijiko kimoja cha siagi na ikishayeyuka chukua mikate yako ya baga uiweke kwenye kikaangio kwa dakika mbili kisha uitoe.

Chukua vipande viwili vya mikate ya baga uhakikishe juu ya kipande kimoja unapaka tomato ketchup kiasi kwa ndani kisha weka jani la lettuce.

Sasa weka kipande kimoja cha nyama kisha paka mayonnaise kiasi juu ya kipande cha nyama. Ongezea kipande cha nyanya ukifuatisha na kipande cha kitunguu.

Bila shaka ni zamu ya kuweka kipande cha jabini kama utatumia. Chukua mkate wa pili weka juu, hapo bugger moja itakuwa tayari kuliwa. Fanya hivyo kwa mikate iliyobaki.

Pakua na ufurahie na kiteremshio ukipendacho.

You can share this post!

IEBC haina nia ya kuhujumu BBI – Chebukati

Nimeshinda urais kwa kura nyingi mno – Bobi Wine