Makala

Jinsi ya kuandaa krimu ya siagi ya kupambia keki

November 20th, 2020 1 min read

Na MARY WANGARI

KEKI ni chakula chenye umaarufu mkubwa mno katika siku za hivi karibuni huku watu wengi wakijifunza jinsi ya kuandaa keki za hafla tofauti.

Kuanzia sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa, kufuzu chuoni, maadhimisho ya harusi, kusherehekea umbali wa tukio fulani na mengineyo, ni bayana kuwa karamu huwa haijakamilika mbapa pale keki itakapokatwa na kuliwa kwa pamoja.

Upishi wa keki ni jambo moja na jinsi ya kuipamba ni jambo jingine linalohitaji weledi wa hali ya juu.

Hata hivyo, kinyume na dhana ya wengi, kuandaa keki si jambo gumu au ghali kwa sababu unaweza kujiandalia wewe mwenyewe jikoni mwako na kufurahia na wapendwa wako hasa msimu wa sherehe za Krismasi unapojongea

Katika ukumbi wetu wa mapishi hii leo, tutajifunza jinsi ya kuandaa krimu ya siagi ya kupambia keki.

Saga krimu yako kwa kutumia mashine ya keki hadi ilainike vyema. Picha/ Mary Wangari

Vinavyohitajika

250 gramu Sukari iliyosagwa au ukipenda Icing sugar (Waweza ukaipata kirahisi dukani)

375 gramu siagi au Blueband kulingana na unavyopendelea.

2 vijiko viwili vikubwa vya maziwa.

11/2 kijiko kikubwa cha arki ya vanilla (Waweza pia kuinunua dukani kirahisi).

Jinsi ya kuandaa

Katika bakuli safi tia siagi na uitwange kwa kutumia mashine ya keki hadi ibadilike rangi na kuwa ya manjano.

Kisha twaa kichungio na uanze kuchekechea unga unga wa sukari yako kwenye bakuli lenye mchanganyiko wa siagi.

Changanya na kusaga unga unga wa sukari uliyochekechea kwenye siagi hadi zichanganyikane vyema na kulainika kwa kutumia mashine.

Baada ya hapo, tia maziwa na uchanganye vyema kwa kutumia mashine.

Ongeza arki ya vanilla kwenye mchanganyiko huo na usage kwa kutumia mashine kwa dakika nne.

Krimu yako sasa ni tayari na uweza kuitumia kupamba na kutia nakshi keki na vitafunio vyako.