Makala

Jinsi ya kufuga kuku wakati wa corona

June 4th, 2020 2 min read

NA PETER CHANGTOEK

JANGA la gonjwa la Covid-19 limekuwa tishio kuu kote ulimwenguni. Kuenea kwa gonjwa hilo, ambalo kwa sasa halina tiba, kumeathiri shughuli nyingi katika takribani nchi zote duniani.

Kufikia wakati huu, watu zaidi ya milioni tano na laki tano wameathirika ulimwenguni. La kutamausha ni kuwa vifo zaidi ya laki tatu vimeripotiwa duniani na vinaendelea kuripotiwa kila kuchao.

Sekta nyingi zimeathirika mno. Kilimo, ambacho ni uti wa mgongo, hakijasazwa na janga hilo na hivyo kuathiri uzalishaji wa chakula.

Hivyo basi, ni jambo bora kwa wakulima kufahamu vyema jinsi ya ‘kucheza kadi’ zao vyema ili kuhakikisha kuwa wanakiendeleza kilimo ipasavyo, na kunufaika kwacho; kwa kupata lishe na fedha pia.

Katika wakati huu ambapo gonjwa hilo linaenea kwa kasi kama moto kichakani, wakulima wanafaa kuwa makini na kujua jinsi ya kuziboresha biashara zao kwa kutumia gharama ya chini huku wakilenga kupata faida na chakula.

Katika makala haya, tunaangazia kinaganaga jinsi wakulima wanavyoweza kuendeleza shughuli za ufugaji wa kuku, na si tu ufugaji, bali ni jinsi wanavyoweza kuendeleza ufugaji bora, hasa wakati huu ambapo korona inatisha.

Ufugaji wa kuku ni mojawapo ya shughuli za zaraa ambazo watu wengi huamua kujitosa kwazo, kwa kuwa wanadhani ni shughuli ambayo haina gharama kubwa mno, ikilinganishwa na shughuli nyinginezo kadhaa za kilimo.

Hata hivyo, kilimo hicho huenda kikamgharimu mkulima fedha nyingi, endapo hatajua jinsi ya kulishughulikia suala hilo kwa umakinifu, uangalifu na ukamilifu.

Wataalamu wanasema kuwa ni jambo aula kwa mkulima kuanza kwa kuwafuga kuku kwa idadi ndogo kabla hajajitosa kuwafuga kuku wengi, hususan endapo mkulima hana maarifa ya kutosha kuhusu kilimo hicho.

Alphonce Otieno ni mmojawapo ya wakulima ambao hujitengenezea lishe za kuku ili kupunguza gharama, hususan wakati huu ambapo pana gonjwa la korona.

Ili kupunguza gharama ya ufugaji, ni jambo mwafaka kwa mkulima kujitengenezea lishe, pasi na kutegemea lishe ambazo huuzwa madukani tu. Kuzitegemea lishe ambazo huuzwa madukani kunaweza kuwa changamoto kuu kwa mkulima, hasa wakati huu ambapo hali ya uchumi imedorora kutokana na gonjwa la korona.

Pia, wataalamu wanasema kuwa ni jambo muhimu kuwalisha kwa lishe zenye virutubisho vyote ili kuboresha uzalishaji na hivyo kumpa mkulima faida tele.

Wataalamu wanafichua kuwa kuku wa kienyeji wanaweza kuboresha ladha ya kuku pamoja na mayai kwa kuwaruhusu kutembeatembea pasi na kuwafungia ndani tu na kuwalisha mumo humo.

David Mutiso, ambaye ni daktari wa mifugo jijini Nairobi, anasema kwamba ni vyema kuwafuga kuku wa kienyeji huku wakiruhusiwa kutembeatembea, kwa kuwa wakiruhusiwa kutembeatembea, misuli yao hunyooka vizuri wanapofanya hivyo, na hivyo basi kuboresha nyama pamoja na mayai kutoka kwa ndege hao.

Aidha, anadokeza kuwa mbinu hiyo ya ufugaji wa kuku wa kienyeji, kwa kuwaruhusu kutembeatembea, husaidia kupunguza visa vya kutokea kwa baadhi ya magonjwa ya kuku, mathalani ugonjwa wa coccidiosis, anaosema kuwa huwaathiri mno kuku wanaofugwa kwa kufungiwa ndani pasi na kupewa nafasi ya kutembeatembea.

Ni jambo aula pia kwa mfugaji kuwakinga ndege wake dhidi ya maradhi, kwa kuwachanja. Vilevile, ni muhimu kuwakinga dhidi ya uvamizi kutoka kwa wanyama na wadudu.

Isitoshe, vibanda vinavyotumiwa kuwafuga vyafaa kujengwa vizuri, na visiwe na baridi, unyevu, joto jingi kupita kiasi, na visiwe na giza totoro, bali viwe na mwanga kiasi.

Wakulima wanafaa pia kutumia mitandao ya kijamii kuyauza mazao yao au bidhaa zao za kilimo. Majukwaa kama vile Facebook, WhatsApp, na mengine mengineyo yana umuhimu sana kwa wakulima, hasa wakati huu ambapo maeneo ya mikusanyiko mathalani masokoni hayana watu.

Kupitia kwa mitandao ya kijamii, wakulima wanaweza kuzitangaza biashara zao na kuwasiliana na wateja wao na kuwasilisha mazao au bidhaa zao kwa wanunuzi pasi na kulazimika kuenda masokoni.