Makala

Jinsi ya kujiandalia chipsi

November 12th, 2020 1 min read

Na DIANA MUTHEU

Muda: dakika 45

Walaji: watu 5

Chipsi ni miongoni mwa vyakula ambavyo vinapendwa na watu wengi haswa wanaoishi mjini, kutokana na wingi wa hoteli na hata vibanda vinavyouza chakula hicho. Kwa mtu yeyote ambaye anapenda chipsi, anaweza kujipikia mwenyewe nyumbani na akafurahia bila kulazimika kwenda hotelini kuinunua.

Vinavyohitajika

1.Viazi kilo 3

2.Mafuta ya kupika lita 1.5

3.Karai ya kukaangia viazi

4.Chumvi

5. Sosi ya nyanya (Tomato sauce)

Jinsi ya kuandaa

Vioshe viazi vyako ili uondoe matope yoyote kisha uvichambue ngozi na uviweke ndani ya maji safi kwa muda wa dakika 15.

Baada ya dakika 15, mwaga maji hayo kisha uvioshe viazi kwa maji mengine safi.

Kata viazi vyote katika umbo la mduara kwanza, kisha uvikate kate tena kwa vipande vilivyo na maumbo sawia na mstatili na uvitumbukize ndani ya maji safi kwa muda wa dakika 5.

Mwaga maji hayo, kisha utumie kichungi kikubwa kukausha maji kabisa katika viazi zako.

Injika karai yako ya kukaangia viazi juu ya moto, kisha uyamwage mafuta yako na uyawache yawe moto sana, kiwango cha kuchemka.

Chukua vipande vyako vya viazi na uvimwage taratibu ndani ya karai yenye mafuta moto, kisha uviwache viive vyenyewe kwa muda wa dakika 15, hadi vikauke vizuri.

Tumia kijiko chenye matundu kuepua viazi vyako ili kuhakikisha mafuta yanachungwa vizuri.

Katika mkebe au sahani unapoweka chipsi zako, tandika kitambaa au serviette ili visaidie kukausha mafuta zaidi katika chipsi hizo.

Waeza andaa pamoja na saladi na soseji.