Makala

Jinsi ya kutengeneza mabuyu

December 16th, 2020 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

Muda wa kuandaa: Dakika 30

Walaji: 3

Vinavyohitajika

sukari vikombe 2

maji vikombe 2

nusu kikombe unga wa ubuyu

vikombe 4 ubuyu wenyewe

pilipili ya unga kijiko ¼

chumvi

iliki ya unga kijiko ¼

rangi nyekundu au yeyote ile utakayopenda.

Maelekezo

Katika sufuria, weka maji na sukari na chumvi na pilipili ya unga na rangi na iliki.

Moto uwe juu kiasi na changanya vyote hivyo vipikike vizuri.

Wakati vitu vinaanza kujipika utakuta rojo linatoa mapovu.

Endelea tu kukoroga acha rojo lipikike vizuri. Baada ya hapo mapovu yakianza kutulia inamaanisha kua rojo limeanza kuwa zito.

Sasa hapo chota kidogo katika mwiko na test kwa vidole kama rojo linanata ua halinati. Rojo linatakiwa linate ndio linakua limeiva. Lisinate sana ila kiasi tu.

Kisha mimina ubuyu wa kokwa na changanya vizuri kabisa katika rojo. Endelea kupika vizuri kama dakika mbili.

Kisha mimina unga wa ubuyu na changanya vizuri tena.

Endelea kupika mpaka unaona sukari inaanza kuganda na kung’aa na kushika vizuri katika ubuyu. Hapo sasa zima jiko na mimina ubuyu katika sinia kubwa na acha ubuyu upoe.

Ukishapoa, ubuyu tayari kuliwa.