Makala

Jinsi ya kutumia viungo asili kuondoa harufu mbaya kwapani

June 5th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

HARUFU ya jasho kwa mwanadamu mara nyingi huhusishwa na uchafu wa mwili.

Hata hivyo, kuna baadhi ya watu ambao kunuka jasho imekuwa kawaida yao licha ya juhudi wanazofanya katika kukoga na kujipaka marashi na manukato mengineyo.

Hali hiyo hutokana na bakteria wanaopatikana katika sehemu za kwapani ambao huchanganyikana na jasho na kusababisha harufu hiyo mbaya; kikwapa.

Kulingana na wataalamu kunuka jasho kupindukia (kikwapa) au (bromhidrosis) inaweza kuwa ni dalili ya ugonjwa na mtu anahitaji ama kuona daktari au kwa baadhi ya watu watumie vitu vya kiasili kukabiliana na kero hiyo.

Kula baadhi ya vyakula kama kabeji au kutozingatia usafi wa mwili aghalabu huhusishwa na harufu kali ya jasho.

Baadhi ya vitu asilia anavyoweza mtu kutumia ili kuondoa harufu hiyo mbaya ni limau au siki ya tunda la tufaha.

Jinsi ya kutumia limau kuondoa harufu ya jasho

Kwanza mtumiaji anafaa kuhakikisha kuwa amenyoa kwapa kisha kuoga kwa maji safi.

Baada ya kuoga anayesumbuliwa na shida hiyo anafaa kukata limau, kisha akachukua kipande kimoja na kusugua kwapani kwa kutumia vipande hivyo.

Atafanya hivyo kila siku hadi pale atakapoona shida ya kunuka imeisha.

Hata hivyo mtu mwenye ngozi iliyo na matatizo hashauriwi kutumia limau kutokana na kemikali iliyo katika tunda hilo.

Jinsi ya kutumia siki ya tufaha

Kutumia kiungo hiki anayesumbuliwa na kikwapa anafaa kuoga na kuhakikisha kuwa amenyoa kwapa.

Kisha atachukua kipande cha pamba na kukichovya katika siki kabla ya kusugua kwapani akitumia pamba hiyo.

Anayetumia atafanya hivyo mara mbili kwa siku hadi pale atakapoona mabadiliko.

Aidha, kuepuka kula vyakula kama kabeji na kuoga mara kwa mara pia kunaweza kusaidia kukabiliana na hali hiyo.