Habari Mseto

Jinsia: Kenya yaorodheshwa moja ya nchi 50 bora duniani

November 14th, 2019 2 min read

Na MARY WANGARI

JUHUDI za Kenya za kuwezesha usawa wa kijinsia zimepigwa jeki huku ikiorodheshwa miongoni mwa mataifa makuu ulimwenguni ikiwemo Canada na Amerika kuhusu uwakilishaji wa jinsia katika utafiti mpya.

Katika ripoti maalum kuhusu usawa wa kijinsia Kenya iliyozinduliwa Jumatatno na shirika la kimataifa la Equileap kwa ushirikiano na New Faces New Voices, pamoja na Soko la Hisa la Nairobi (NSE), benki ya Standard Chartered iliongoza nchini kama kampuni yenye kiwango cha juu zaidi cha uwakilishaji wa kijnsia.

Kampuni hiyo iliongoza katika orodha ya kampuni 10 bora zaidi nchini Kenya kwa asilimia 63, na pia kutajwa miongoni mwa mashirika 50 bora zaidi ulimwenguni, kuhusu usawazishaji wa idadi ya wanawake na wanaume katika mazingira ya kazi.

Kulingana na mkurugenzi wa Equileap Diana van Maasdijk, utafiti huo ulihusisha kampuni 3,500 kutoka mataifa 23 yanayoedelea duniani ambapo uliangazia vipengele vinne vya uwakilishaji ikiwemo: bodi, mkurugenzi, msimamizi mkuu na wafanyakazi.

Kampuni nyinginezo bora kuhusiana na uwasawazishaji wa jinsia ni pamoja na: WNN Scan Group, Safaricom, Benki ya Barclays, Kenya Airways, Kenya Re, Kengen, Stanbic, KCB na East African Breweries mtawalia.

“Idadi kubwa ya wanawake wanafanya kazi katika sekta zisizo rasmi. Lakini hali hiyo itabadilika hivi karibuni maadamu wanawake zaidi wanajiunga na sekta rasmi,” alisema Bi Maasddijk.

Kulingana na Katibu Mkuu katika Wizara ya Huduma ya Umma Rachel Shebesh aliyehudhuria hafla hiyo, serikali ilikuwa imepiga hatua kuu chini ya utawala wa rais Uhuru Kenyatta katika usawazishaji wa jinsia.

“Ni mara ya kwanza tunashuhudia kuwa na viongozi wanawake katika wizara zilizochukuliwa kuwa himaya za wanaume. Tatizo si sera, maadamu sheria kadha zimebuniwa, shida ipo katika utekelezaji wa sera hizo kuhusu wanawake,” alisema Bi Shebesh.

Mwenyekiti wa New Faces New Voices Kenya Andia Chakava, alieleza kuwa utafiti huo unaashiria mabadiliko yanayotarajiwa kuhusu idadi ya wanawake katika sekta rasmi kwa kipindi cha miaka 20 ijayo.

“Lengo la utafiti huu ni kusaidia viongozi wa biashara kuelewa mashirika yao na kuwezesha waunda sera kulenga vyema miradi inayozingatia jinsia,” alisema Bi Chakava.