Makala

JIPODOE: Changanya asali, limau na papai ili kuondoa madoa usoni na sehemu zingine mwilini

September 7th, 2019 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

KUMEKUWA na sababu mbalimbali zinazofanya watu kutokuwa na ngozi nyororo.

Kubadilika kwa hali ya hewa, matumizi ya pombe na sigara, na hata matumizi ya krimu kali ambazo baadhi ya watu huzitumia bila kujua madhara yake, ni baadhi tu ya sababu za kuharibika kwa ngozi.

Ngozi kwa kawaida inatakiwa ijitengeneze yenyewe na si kuitengeneza kwa vipodozi kama wengi wanavyodhani.

Ulaji wa matunda na mboga za majani kwa wingi na kunywa angalau glasi nane za maji kila siku ni njia nzuri kama unataka kuwa na ngozi nzuri isiyo na madoa, vidutu na ukavu ambao haupendezi.

Wengi wameacha kula mbogamboga na matunda kwa wingi na hata kutokunywa maji ya kutosha na huku wakitarajia kuwa na ngozi nzuri. Basi kuanzia leo wanafaa wajue kwamba ni vigumu ndoto yao kutimia wakati wanafanya mambo kinyume.

Vipo visa kadhaa vya watu wanaopaka krimu kali kuishia kuungua usoni huku ambapo miili yao inaonekana kuwa kavu.

Hali hii inaashiria kuwa kupaka krimu si suluhisho la kuwa na ngozi nzuri.

Kwa upande mwingine, kuna watu walio na ngozi za asili na hata unapowauliza, baadhi yao hawajawahi kupaka krimu hata siku moja na bado wana ngozi nzuri zinazovutia. Hao bila shaka wamekuwa wakila kwa ajili ya kuhakikisha wanatengeneza ngozi zao kutoka ndani.

Pia wengi wanaharibu ngozi zao na kuishia kuwa na madoa kutokana na kutumia vipodozi kwa muda mrefu na hata wanapogundua kuwa wana matatizo hayo wanaanza kubadilisha krimu wakidhania ndio suluhu. Matokeo yanakuwa ni madhara makubwa kwenye ngozi zao.

Unaweza kutibu ngozi yenye madoa usoni  pia mashavuni kwa kujitibu na papai.

Namna ya kufanya

Chukua limau, lioshe na kisha likamue na kuchuja kuondoa mbegu zake.

Mimina juisi hiyo kwenye kikombe safi na kisha changanya na vipande vya papai vilivyopondwa. Tafuta kitambaa laini na nyororo kisha kichovye kwenye mchanganyiko huo na upake kwenye sehemu zenye tatizo.

Kaa kama dakika tano kisha osha uso kwa maji safi.

Pia unaweza kuchanganya asali na mchanganyiko wa papai.

Limau lina sifa kubwa ya kuzuia harufu mbaya. Hii ina maana kwamba unaweza kulitumia katika kuondoa harufu kali ya jasho mwilini na husaidia kuondoa weusi kwenye kwapa, chini ya macho na mapajani pia. Chukua kipande cha limau, mimina sukari kiasi, kisha litumie kama sponji ya kusugua sehemu ya ngozi.

Unatakiwa kutumia kwenye kwapa ambalo ni safi kabla na baada ya kuoga.