Habari Mseto

Jirani alisafiri akaniambia nimwangalilie jamaa zake, najiuliza kama nimtunzie mke pia

January 10th, 2024 1 min read

Hujambo shangazi? Jirani yangu alisafiri ugenini kikazi mwaka uliopita. Aliniomba niwe nikitembelea familia yake kuijulia hali. Mkewe ni mchanga na nina hakika mwili unamsumbua. Nitakosea kumsaidia?

Mawazo yako hayo yanaongozwa na tamaa. Jirani yako alikutuma kwa sababu anakuamini. Pili, mkewe hajakwambia anahitaji msaada wako. Kama hutaki aibu, achana na mpango huo.

Nimeolewa mke wa pili, mume wetu naye amelemewa na kazi ya chumbani, nifanyeje?

Nimeolewa mke wa pili. Mume wetu ana miaka 55 na ameanza kulemewa na kazi ya chumbani. Mara nyingi akija kwangu huwa ni kulala tu. Mimi bado ni mchanga, nishauri.

Hiyo ni mojawapo ya changamoto za mwanamume kuwa na wake zaidi ya mmoja. Katika umri wake huo ameishiwa na nguvu, hana uwezo hata wa kumtosheleza mke mmoja. Kama unahisi huwezi kuvumilia una haki ya kuondoka.

Tunakosana mara nyingi na mchumba, sasa nahisi hatuwezi kuwa wanandoa

NIMEKUWA nikikosana na mpenzi wangu kuhusu mambo madogo tu. Wakati mwingine hata tumeapa kuachana lakini hatimaye tunajipata pamoja tena. Sitaki hali iwe hiyo tukioana. Waonaje?

Hali kwamba mmeshindwa kuachana licha ya ugomvi wenu ni ishara kuwa mapenzi yenu ni ya dhati. Jinsi pekee ya kumaliza ugomvi ni kutambua na kuepuka mambo yanayowafanya mkosane. Shauriana na mpenzi wako.

Nampenda mume sana, kuna ubaya nimpe dawa ya kukolezi penzi letu?

Nimeolewa na mwanamume aliyekamilika kwa kila namna na nimejitolea kumkinga kwa vyovyote vile dhidi ya wanawake wengine. Nitakosea kutafuta dawa?

Usitupe pesa zako kwa waganga eti unatafuta dawa ya kumkinga mume wako. Dawa pekee ya kumfumba macho mwanamume huyo ni kumkoleza mapenzi tu. Kazi kwako.