Habari Mseto

Jiuzulu ujipange kuwania Ugavana Nyeri, Gachagua aambiwa

June 10th, 2024 2 min read

SHABAN MAKOKHA NA LABAAN SHABAAN 

BAADHI ya wandani wa Rais William Ruto wa eneo la Magharibi wanamtaka Naibu Rais Rigathi Gachagua ajiuzulu na angoje Uchaguzi Mkuu wa 2027 ili agombee kiti cha ugavana Nyeri.   

Wanasiasa hao wakiongozwa na Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa, wamemlaumu Naibu Rais wakisema anachochea siasa za ukabila licha ya kuwa kiongozi wa kitaifa.

Mbunge huyo amemwambia Bw Gachagua amheshimu Rais Ruto na atulie kwa sababu anahudumu katika wadhifa ambao anadai ulifaa kuwa wa Waziri wa Usalama, Kithure Kindiki.

Akimtaja Naibu Rais kuwa mkabila, Bw Barasa alimjaribu Bw Gachagua akimtaka ajiuzulu iwapo anahisi amesumbuliwa anaposhirikiana na Rais Ruto.

Mbunge huyu amemwelekeza Naibu Rais abwage zana za kazi kasha asubiri kuwania ugavana Nyeri 2027.

“Tunataka maendeleo kuenea katika kaunti 47 bila kujali idadi ya watu katika maeneo hayo. Baadhi ya wahusika wanaotaka kuturudisha nyuma lazima watupiliwe mbali mara moja,” alisema Bw Barasa katika kijiji cha Namwela huko Sirisia, Bungoma wakati wa mazishi ya Bw Morris Simiyu, babake Mercy Simiyu wa Shirika la Habari la Nation Media Group.

Bw Barasa amemshutumu Bw Gachagua akisema ameanza kampeini za mapema kumrithi Rais Ruto licha ya wao kuhudumu katika serikali moja.

Mbunge huyo alijuta kumuunga mkono Bw Gachagua kama mgombea mwenza wa Rais Ruto akidai kuwa Naibu Rais amekaidi matakwa ya serikali anapovumisha kampeini ya ugavi mapato kwa misingi ya Mtu mmoja, Kura moja na Shilingi moja.

“Bw Gachagua anafaa kufanya uamuzi iwapo atasimama na Rais William Ruto kutimiza ahadi walizotoa kwa Wakenya wakati wa kampeni au ajiuzulu na kuwa kinara katika siasa za Mlima Kenya. Si busara kwa Bw Gachagua kujishughulisha tu na ustawi wa eneo lake la asili, licha ya kuwa katika kiti cha Urais, ambacho ni ishara ya umoja wa kitaifa,” mbunge huyo alisema.

Mbunge wa Sirisia John Waluke ambaye pia alihudhuria hafla ya mazishi, alitoa changamoto kwa Bw Gachagua akimwambia ajitolee kutetea ustawi wa nchi nzima na kuacha kujihusisha tu na ngome yake ya Mlima Kenya.

“Kama Naibu wa Rais, Gachagua alifaa kujua zaidi ya wengine kuwa yeye ni kiongozi wa kitaifa na wala si mfalme wa eneo. Iwapo anahisi kwamba hafurahii wadhifa anaoshikilia, basi ajiuzulu na aende kuwania kiti cha eneo la Nyeri,” alifoka Bw Waluke.

Kuhusu kampeni ya Mtu Mmoja, Kura Moja, Shilingi Moja, Bw Barasa aliteta kuwa Magharibi inaongoza kwa idadi ya watu na inafaa kupewa kipaumbele cha kwanza ukiwa wito wa Bw Gachagua ni sawa.

Bw Gachagua ambaye anakabiliwa na mashambulizi makali ya kisiasa kutoka kwa wanasiasa wa ngome yake ya Mlima Kenya, amesalia na kibarua cha kuongeza uungwaji mkono katika juhudi zake za kuibuka kinara wa ajenda ya maendeleo ya eneo hilo.

Kadhalika, ameendelea kukaidi wito wa Rais Ruto wa kuwataka viongozi kujiepusha na kuendeleza ‘siasa za ukabila.’

Bw Gachagua amekariri kuwa kuna njama ya viongozi walio karibu na Rais kumtenga ili wao wajihusishe na kupanga siasa za Mlima Kenya. Naibu Rais anasema siasa hizi haziwahusu viongozi hao wa eneo la Bonde la Ufa.

Tangu alipotangaza azma yake ya kuunganisha eneo la Mlima Kenya na kujipigia debe kuwa kinara wa eneo hilo kupitia mpango wa ugavi mapato, Bw Gachagua amekabiliwa na cheche kali za kisiasa ndani ya chama cha UDA.