Habari

JLAC yamuidhinisha Ann Nderitu awe msajili wa vyama vya kisiasa

September 24th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KAMATI ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) imeidhinisha uteuzi wa Ann Nderitu kuwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa.

Katika ripoti iliyowasilishwa bungeni Alhamisi asubuhi, na mwenyekiti wa Kamati hiyo Muturi Kigano, wanachama wa kamati hiyo walisema kuwa wameridhika kuwa Bi Nderitu amehitimu kwa wadhifa huo muhimu.

“Baada ya kumpiga msasa Bi Nderitu wiki jana, kamati hii imeridhika kuwa amehitimu kuendesha majukumu ya afisi ya msajili wa vyama vya kisiasa. Tumeshawishika kuwa amehitimu na anayo tajriba kwa kazi hiyo muhimu,” Bw Muturi akasema kwenye taarifa iliyoandamanishwa na ripoti hiyo.

Bi Nderitu amekuwa akihudumu kama Kaimu Msajili wa Vyama vya Kisiasa tangu 2018 alipochukua wadhifa huo kutoka kwa Lucy Ndung’u ambaye alihamishwa hadi Tume ya Kupokea Malalamishi ya Umma (CAJ) kuhudumu kama kamishna. Bi Ndugu pia alishikilia wadhifa huo kama kaimu, kwa miaka minane.

Uteuzi wa Bi Nderitu ukiidhibishwa na bunge, atakuwa mtu wa kwanza kuhumu kama Msajili kamili wa vyama vya kisiasa tangu Katiba ya sasa ilipozinduliwa rasmi.

Wakati huo huo, kamati ya JLAC iliidhinisha uteuzi wa Florence Tabu na Ali Abdullahi kuwa naibu msajili wa vyama vya kisiasa. Hata hivyo, Muturi na wenzake walikataa kuidhinisha uteuzi wa Wilson Mohocho ambaye pia alipendekezwa na Rais Uhuru Kenyatta kuwa naibu msajili wa vyama vya kisiasa.

Rais Kenyatta alipendekeza uteuzi wa wanne hao mnamo Septemba 8, 2020 na kuwasilisha majina yao bungeni.

Kabla ya kuchukua wadhifa huo, kama kaimu, Bw Nderitu alihudumu kama Mkurugenzi wa Usajili wa wapiga kura katika Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).