Michezo

Jobita ahakikishia mashabiki usimamizi kurejesha uthabiti Western Stima

August 29th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

LICHA ya wanasoka wengi tegemeo kuagana na Western Stima, mwenyekiti Laban Jobita ameshikilia kwamba mustakabali wa kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Kenya (KPL) hautazimika na usimamizi utajitahidi kurejesha uthabiti wa awali.

Matumaini ya Stima ya kushindana vilivyo kwa kiwango sawa na wapinzani wao katika soka ya humu nchini yalididimizwa zaidi na hatua ya wadhamini wao, kampuni ya umeme ya Kenya Power, kusitisha ufadhili wao mnamo Juni.

Vikosi vingi vya KPL vilichuma nafuu kutokana na hali tete ya kifedha kambini mwa Stima na wamesajili takriban wanasoka wote wa haiba kubwa na kutikisa benchi ya kiufundi ya klabu hiyo.

Katika mahojiano yake na Taifa Leo, Jobita amesisitiza kuwa Stima wameingia mkataba na shirika moja litakalosimamia sasa shughuli zote za kusajili wachezaji wapya muhula huu.

Kati ya wanasoka ambao wameagana rasmi na Stima hadi kufikia sasa ni Stephen Odhiambo, Edwin Omondi na Maurice ‘Fadha’ Ojwang ambao wameyoyomea Wazito kwa pamoja na kocha wao Salim Babu. Weingine ni Abdalla Wankuru, Benson Omalla, Kelly Wesonga na Fidel Origa.

“Tutasajili chipukizi wengi hivi karibuni na kuunda kikosi kipya tutakachokitegemea kuanzia msimu ujao. Hakuna namna ambavyo Stima itakubali kuyumbishwa ilhali tumezingirwa na idadi kubwa ya chipukizi wanaojivunia utajiri wa talanta na vipaji vya kutandaza soka,” akasema mchezaji huyo wa zamani wa Kisumu Hot Stars na Gor Mahia.

Hata hivyo, Jobita amefichua kwamba itawalazimu kupunguza kabisa kiwango cha mishahara ya wachezaji wao hadi watakapopata mdhamini mpya.

“Changamoto kubwa ni kwamba hatutaweza kulipa mishahara na marupurupu kama zamani. Hata tukifaulu kusalia na baadhi ya wachezaji tuliowategemea hapo awali, itatujuzu kuwapunguzia posho,” akaongeza.

“Wote wanaotaka kuagana nasi wako huru kufanya hivyo ila kwa kuzingatia taratibu zote zilizopo. Sera zetu haziwezi kuturuhusu kumkwamilia mchezaji ambaye anahisi atapiga hatua kubwa zaidi kitaaluma akivalia jezi za kikosi kingine,” akasisitiza Jobita.

Ojwang, ambaye pia amewahi kuchezea Gor Mahia, ndiye mchezaji wa hivi karibuni kutambulishwa rasmi kwa mashabiki wa Wazito waliotema jumla ya wanasoka 12 mwanzoni mwa Julai.

Beki huyo ni mchezaji wa nne kusajiliwa na Wazito kutoka Stima na ni sogora wa 11 kuingia kambini mwa mabwanyenye hao ambao kwa sasa wananolewa na kocha Fred Ambani kwa usaidizi wa Babu.

Babu alianza ukufunzi wake katika kikosi cha mabingwa wa KPL 2006, SoNy Sugar akiwa kocha msaidizi. Alikwezwa baadaye kuwa mkufunzi mkuu kabla ya kuyoyomea Migori Youth kisha Stima walioagana naye Agosti 10.

“Ojwang ni beki aliye na uwezo wa kutamba katika nafasi yoyote kwenye safu ya ulinzi. Ujio wake ni nafuu tele kwa kikosi,” akasema Ambani.