Habari

Joe Kadenge anazikwa leo

July 20th, 2019 1 min read

Na DERICK LUVEGA

MAREHEMU Joe Kadenge ambaye aliizolea Kenya sifa katika mchezo wa kandanda anazikwa leo Jumamosi.

Tayari maombi kabla ya mazishi yanaendelea katika Shule ya Msingi ya Gisambai, Kaunti ya Vihiga.

Mamia ya waombolezaji wamehudhuria maombi hayo yanayoongozwa na Kanisa la Friends Church.

Mamia ya waombolezaji Julai 20, 2019, katika Shule ya Msingi ya Gisambai. Picha/ Isaac Wale

Kuna skrini kubwa ambazo zimewekwa ili waombolezaji wafuatilie kila tukio.

Mtangazaji maarufu Jack Oyo Silvester ni miongoni mwa watu maarufu waliotoa salamu za pole ambapo amemmiminia sifa Kadenge.

Amesema wakati wa uhai wake, Kadenge aliishi katika miji mbalimbali tangu aanze kuichezea timu ya taifa Harambee Stars mwaka 1956.

“Zama hizo Kadenge akiichezea Harambee Stars, walikuwa wanawania Gossage Cup (kwa sasa Cecafa). Kombe hilo liliitwa Gossage kwa sababu wadhamini walikuwa ni kampuni ya sabuni ya Gossage ya nchini Amerika,” amesema Jack Oyo Silvester.

Mwanasoka huyo mstaafu aliyekuwa na umri wa miaka 84 aliaga dunia Julai 7, 2019.

Alikumbana na mauti wakati akitibiwa katika hospitali moja jijini Nairobi baada ya kuzidiwa na maumivu ya kiharusi.