Michezo

JOGOO WA JIJI: Manchester United yaizidi maarifa Manchester City

March 10th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, UINGEREZA

KOCHA wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer asema ni heshima kubwa kwake kudhibiti chombo cha Red Devils kwa sasa, baada ya vijana wake kugaragaza mahasimu wao wa jadi, Manchester City katika mikondo miwili ya ligi kwa mara ya kwanza katika miaka 10.

Man-United waliwapepeta Man-City 2-0 uwanjani Old Trafford, Jumapili katika mechi iliyokuwa ya 50 ya ligi kwa Solskjaer tangu apewe mikoba ya Red Devils.

Ushindi huo unafuatia kichapo cha 2-1 ambacho Man-United waliwapa majirani hao uwanjani Etihad katika mkondo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mwezi Desemba.

Ni mara ya kwanza kwa Man-United kufikia ufanisi huo tangu msimu wa 2009/10 chini ya mkufunzi wao wa muda mrefu (miaka 27), Sir Alex Ferguson ambaye alistaafu mnamo 2013.

Ushindi wa Jumapili pia uliwaacha Liverpool wakijivunia pengo la alama 25 kileleni mwa jedwali la EPL, mbele ya bingwa mtetezi Man-City.

Ina maana kwamba Liverpool sasa wanahitaji kuvuna ushindi mara mbili pekee katika mechi tisa zilizosalia ili kutawazwa wafalme wa EPL kwa mara ya kwanza katika miaka 30.

Man-United nao waliweka hai matumaini ya kufuzu kwa kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao, sasa wakishikilia nafasi ya tano katika EPL kwa alama 45, tatu nyuma ya Chelsea wanaofunga orodha ya nne-bora kuingia UEFA.

Zaidi ya kuwanyamazisha majirani wao, Solskjaer alisema matamanio yake ni kuongoza Man-United kukamilisha kampeni za EPL ndani ya mduara huo wa nne-bora.

Ushindi wa Jumapili ulichangiwa zaidi na masihara ya kipa Ederson Moraes, ambaye kocha Pep Guardiola amemsuta na kumtaka amakinike zaidi katika michuano miwili ijayo dhidi ya Arsenal na Real Madrid.

Kutomakinika kwa Ederson kuliwapa Man-United bao la kwanza kupitia Anthony Martial, kabla ya Scott McTominay kushirikiana vilivyo na Bruno Fernandes kutikisa nyavu za wageni wao mwishoni mwa kipindi cha pili.

Kufikia sasa, Man-United hawajapoteza mchuano wowote kati ya 10 iliyopita; wameshinda tatu na kuambulia sare tatu.

Hii ndiyo rekodi ndefu zaidi ya Solskjaer bila kushindwa tangu awaongoze waajiri wake kupiga mechi 11 bila kujikwaa, pindi alipopokezwa mikoba kama kaimu kocha mnamo Desemba 2018.

Kwa upande wake, ni mara ya pili kwa Gaurdiola kuzidiwa maarifa mara tatu na mpinzani mmoja chini ya msimu mmoja katika historia yake ya ukufunzi. Kocha huyo Mhispania alionja shubiri hiyo kwa mara ya kwanza dhidi ya Liverpool mnamo 2017-18.

Martial sasa ndiye mchezaji wa pili wa Man-United kufunga bao katika debi tatu mfululizo za Manchester, wa kwanza akiwa Eric Cantona aliyefunga katika msururu wa debi tano kati ya Machi 1993 na Aprili 1996.

Tangu avalie jezi ya Man-United katika mechi yake ya kwanza ugani Old Trafford mnamo Februari 1, Fernandes amefunga mabao mawili na kuchangia mengine matatu.

Gozi la Jumapili lilimfanya fowadi Raheem Sterling wa Man-City kuwa mchezaji wa nne mchanga zaidi – baada ya Wayne Rooney, James Milner na Gareth Barry – kuwahi kutandaza jumla ya mechi 250 za EPL.

Baada ya kupepetana na Arsenal kesho ugani Etihad, Man-City watavaana na Burnley nyumbani kabla kualika Real kwa mkondo wa pili wa mechi ya UEFA.

Nao Man-United watakuwa wageni wa Linzer Athletik-Sport-Klub (LASK) ya Austria katika Ligi ya Uropa siku ya Alhamisi kabla kuwaendea Tottenham Hotspur ligini mwisho wa wiki.

MATOKEO YA EPL (Jumapili):

Chelsea 4-0 Everton

Man-Utd 2-0 Man-City