Habari

John De' Mathew anazikwa leo Jumamosi

August 24th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

KUFIKIA saa mbili asubuhi, mamia ya mashabiki wa mwanamuziki marehemu John De’ Mathew wamekuwa wamekusanyika katika mochari ya Chuo Kikuu cha Kenyatta ambapo mwili wake umehifadhiwa.

Nyumbani kwa marehemu katika Kaunti ya Murang’a, hali ni iyo hiyo ambapo mamia ya waombolezaji wameanza kufika ili kuwa kushuhudia kwa kweli John Mwangi Ng’ang’a ambaye ndiye huyo De’ Mathew ameshaiaga dunia.

Wengi walianza kuwasili katika hifadhi hii ya wafu na pia kwake nyumbani mwendo wa saa 12 asubuhi wakiabiri magari, wakitembea kwa miguu na wengine juu ya pikipiki wakiwa na matumaini ya kuutazama mwili na wakikosa, wapungie jeneza lake mkono wa heri njema akienda zake kuzimu.

Katika ratiba ya mazishi utazamaji mwili wa mwendazake umetengewa kati ya saa moja na saa 12 asubuhi.

Mwanamuziki huyo alifariki Jumapili mwendo wa saa tatu na nusu katika ajali ya barabara karibu na Mkahawa wa Blue Post, kaunti ya Kiambu.

Kwa miaka 33, De Mathew aliwaburudisha mashabiki wake kwa lugha ya Gikuyu na ambapo ameacha nyuma zaidi ya awamu 50 za kanda za nyimbo za kimapenzi, ushauri wa kijamii na siasa.

Ijumaa, Taifa Leo ilitembelea kaunti ndogo ya Gatanga katika kijiji cha Mukurweini ambapo mwili wa De’ Mathew unasafirishwa kuzikwa.

Kwa mujibu wa gavana wa Murang’a, Mwangi wa Iria, serikali ya kaunti na ile ya kitaifa zimeshirikiana kuandaa mazishi hayo.

“Rais Uhuru Kenyatta ambaye alikuwa rafiki wa dhati amejitolea kugharimia mazishi haya kwa kiwango kikuu, serikali yake ikishirikisha pia masuala ya usalama wa waombolezaji watakaojitokeza na serikali ya kaunti ikichangia uchimbaji na kukoroga simiti ya kaburi na pia kukarabati barabara za kuingia na kutoka katika boma la mwendazake,” akasema Wa Iria.

Aidha, ni mazishi ambayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na watu mashuhuri, Rais akiwajibikia heshima zake za mwisho kwa mwendazake, Naibu Rais, Dkt William Ruto ambaye alikuwa amejishindia uungwaji mkono wa De’ Mathew katika ari yake ya kuwa Rais baada ya uchaguzi wa 2022 akitarajiwa, Raila Odinga na Kalonzo Musyoka pia wakitajwa kuwa yapo matarajio yao ya kujitokeza kumzika mwanamuziki huyo.

Wengine ni wanasiasa wa Murang’a na wengine kutoka nje ya eneo hilo, Mbunge wa Soi Caleb Kipkemei Kositany akiwa wa kipekee akimwakilisha Dkt Ruto katika kamati nne za kuandaa mazishi.

Taifa Leo itakuangazia hali itakavyokuwa na itakavyosihia katika hafla hii ambapo hafla ya maombi na hotuba itaandaliwa katika shule ya msingi ya Githambia na ambayo De’ Mathew alisomea miaka 44 iliyopita, wakati huo ikifahamika kama Mukurwe.

Baadaye, mazishi yatafanyika katika hafla ndogo katika shamba lake na wajane wake wawili pamoja na watoto wao saba.

Mungu mwenye nguvu dhidi ya uhai na mauti ndiye ajuaye kisa na sababu katika maisha ya De’ Mathew ambaye jina lake milele litabakia kwa nyoyo za mashabiki wake.

Tunafuatilia shughuli zote hizi na baadaye, tutakupa habari kamili kuhusu mazishi haya na ambayo yatapeperushwa moja kwa moja na runinga kadhaa hasa zile za kuandaa vipindi kwa lugha ya Gikuyu.