Michezo

John Kiplangat tayari kwa makala ya saba ya mbio za Deaf Half Marathon

November 7th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

WANARIADHA watakaoshiriki mbio za Deaf Half Marathon mwaka huu sasa wana kipindi cha chini ya mwezi mmoja pekee kujiandaa kwa makala ya saba ya kivumbi hicho kitakachofanyika Disemba 6, 2020 jijini Nairobi.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Riadha la walemavu wasio na uwezo wa kusikia nchini Kenya (DAAK), maandalizi kwa minajili ya mbio za Deaf Half Marathon yameshika kasi na mashindano hayo yataendeshwa kwa mujibu wa kanuni zilizotolewa na Wizara ya Afya na ile ya Michezo kuhusu jinsi ya kudhibiti msambao wa Covid-19.

“Tumeanza matayarisho kwa kuchelewa kidogo. Hata hivyo, tunatarajia kufanikisha mbio hizo kwa wakati baada ya kupata msaada kutoka kwa mashirika mbalimbali,” akasea Tom Okiki ambaye ni Afisa wa Mahusiano wa DAAK.

Iwapo mambo yatakwenda jinsi yalivyopangwa, basi mbio za Deaf Half Marathon zitakuwa za kwanza miongoni mwa walemavu wasio na uwezo wa kusikia kuandaliwa humu nchini tangu Machi 2020 ambapo shughuli za michezo zilisitishwa kwa sababu ya Covid-19.

Awali, mbio za Deaf Half Marathon zilitarajiwa kufanyika Aprili 26, 2020 mjini Nakuru huku mashindano mengine ya ukumbini na uwanjani miongoni mwa wanariadha hao wasio na uwezo wa kusikia yakiratibiwa kufanyika katika uwanja wa MISC Kasarani kati ya Mei 29-30, 2020.

“Japo Safaricom wamekubali kudhamini kampeni za mwaka huu, kiwango cha ufadhili wao kitatuwezesha kushirikisha wanariadha wa haiba kubwa pekee,” akasema Okiki.

Mnamo 2019, mtimkaji Daniel Kiptum wa Kaunti ya Nandi aliibuka mshindi wa Deaf Half Marathon kwa muda wa saa 1:11.16 na kuhifadhi ufalme wa taji hilo kwenye mashindano yaliyofanyika katika Kaunti ya Kericho. Taji la wanawake lilimwendea Juster Moraa Kwamesa aliyefika utepeni baada ya muda wa saa 1:42.01.

Mbio za mwaka huu zimemvutia pia mwanariadha John Kiplangat aliyenyakua nishani ya dhahabu katika mbio za mita 1,500 mnamo 2017 katika mbio za Deaflympics nchini Uturuki kabla ya kutawala mashindano ya Africa Deaf Championships mnamo 2019 jijini Nairobi.

“Kwa sasa najitahidi kadri ya uwezo wangu kushiriki mazoezi kabambe ili kujiweka sawa kwa mashindano yajayo. Tatizo la pekee ni kwamba hakuna kambi ya mazoezi kwa watu wasio na uwezo wa kuona hapa Narok,” akasema Kiplangat ambaye alikuwa miongoni mwa wanariadha waliotambuliwa na kutuzwa na Rais Uhuru Kenyatta katika sherehe za kuadhimisha Sikukuu ya Mashujaa Dei mnamo Oktoba 20, 2020 katika Kaunti ya Kisii.