Michezo

John Obi Mikel arejea katika soka ya Uingereza kuvalia jezi za Stoke City

August 17th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Stoke City kinachoshiriki Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Uingereza (Championship) kimemsajili nahodha wa zamani wa Super Eagles ya Nigeria, John Mikel Obi, 33 kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Mikel ambaye pia amewahi kuvalia jezi za Chelsea, alisalia bila klabu baada ya kuagana rasmi na Trabzonspor ya Uturuki mnamo Machi 2020.

Kusajiliwa kwa Mikel kunatokea siku mbili baada ya kukiri kwamba alikuwa radhi zaidi kurejea kusakata soka ya Uingereza.

Akiwa mwanasoka wa EPL, Mikel aliwajibishwa na Chelsea mara 249 katika kipindi cha miaka 11.

Aliondoka uwanjani Stamford Bridge mnamo 2017 baada ya kushindia waajiri wake ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), mataji mawili ya EPL, makombe matatu ya FA na taji moja la Carabao League Cup.

Baadaya kukatiza uhusiano na Chelsea, aliyoyomea China kuvalia jezi za Tianjin TEDA kabla ya kuingia katika sajili rasmi ya Middlesbrough nchini Uingereza kwa kipindi kifupi mnamo 2019.

Hadi alipotangaza kustaafu rasmi kwenye soka ya kimataifa, Mikel alikuwa amewajibishwa na timu ya taifa ya Nigeria mara 89.

Aliongoza kikosi hicho cha Super Eagles kwenye fainali mbili za Kombe la Dunia na akakisaidia kunyanyua ubingwa wa Kombe la Afrika (AFCON) mnamo 2013 nchini Afrika Kusini.

Stoke City walisajili ushindi kwenye mechi tatu kati ya nne za mwisho katika kivumbi cha Championship msimu huu wa 2019-20 na kukwepa shoka ambalo vingnevyo lingewateremsha ngazi hadi Daraja la Pili (League One).

Kikosi hicho kiliambulia nafasi ya 15 chini ya kocha wa zamani wa Ireland Kaskazini, Michael O’Neill.