Makala

JOHN OGO: Msanii ibuka anayelenga kuwapa matumaini wanaougua Ukimwi

April 18th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

AMEPANIA kutumia utunzi wa nyimbo zake kubadilisha maisha ya wengi hapa nchini. Anaamini ni kipaji alichotunukiwa na Mungu maanake alianza kujituma kwenye masuala ya muziki tangu akisoma Shule ya Msingi ya Waondo, Kaunti ya Homabay.

Kadhalika ni talanta anayolenga kuikuza ili kufikia viwango vya wanamuziki mahiri katika nyimbo za injili kama Rose Muhando na Christina Shusho kati ya wengine.

John Onyango Ogo, msanii chipukizi ambaye kitaaluma licha ya kuhitimu kwa shahada ya diploma katika masuala ya biashara yeye ni mlinzi chini ya kampuni moja jijini Nairobi.

”Mimi nafanya kazi ya ulinzi yaani ‘usoja’ kama wengi wanavyopenda kusema lakini nashukuru Mungu maanake kwa neema yake anafahamu alichonipangia maishani mwangu,” aliambia Taifa Leo Dijitali.

Ni mtunzi wa nyimbo za kizazi kipya anayetumia mtindo wa Rhumba kueneza injili ya Mungu. “Nilianza utunzi wangu mwaka 2012 ingawa sikufahamu kwamba ilikuwa talanta niliyohitaji kuikuza maana mara nyingi nikienda kulala nilikuwa najipata naimba hadi natoa machozi,” alisema na kuongeza kuwa analenga kujituma kwa udi na uvumba ili kutinga levo nyingine.

John Ogo akicheza na wanadensi wake wa injili katika mojawapo ya nyimbo zake. Picha/ YouTube

Msanii huyu mwenye umri wa miaka 28 anasema aliokoka mwaka 2009 baada ya kupitia kipindi kigumu ambapo aliteswa kwa muda na ugonjwa wa goita hali iliyomfanya kujipeana kwa Mungu kumuongoza maishani mwake. Anadokeza kuwa Mungu ndiye mchungaji na mwokozi wake maishani (Zaburi 23).

Anakiri kwamba katika wokovu kuna mengi ya kujivunia ikiwamo furaha, upendo na amani hata wakati kimaisha unajihisi kutofikia kiwango unachohitaji maana ukiwa ndani ya Kristo hakuna kisichowezekana.

Tayari chipukizi huyu amefaulu kurekodi nyimbo tano, ‘Shujaa Wangu’ na ‘Mwamba Wangu’ (zote video) nazo audio zikiwa ‘Kombolewa’, ‘Nyasach Elijah’ na Jehova Shalom.’

”Kwa neema yake Mwenyezi Mungu najitahidi niwezavyo nihakikishe nimetoa video za nyimbo hizo tatu ili ujumbe wake uwafikie wengi nchini,” alisema na kuongeza kwamba anapenda sana kutunga nyimbo za kuwapa imani waliovunjika kiroho.

Anasema kuwa pia hupenda kujifunza kutoka kwa wengine waliopiga hatua katika muziki wa injili ambapo huchukua muda kusikiza kazi za waimbaji kama Everline Wanjiru ‘Mungu Mkuu’ na ‘Tunakuabudu,’ pia wake Gloria Muliro ‘Ndiyo Yako,’ na ‘Narudisha’ kati ya wengine.

Hapa, anaonyesha miondoko ya kumsifu Mola katika video ya kibao ‘Mwamba Wangu’. Picha/ YouTube

Pia Afrika Mashariki anapenda kusikiza kazi za waimbaji kama Rose Muhando ‘Wololo’ na ‘Ndivyo Ilivyo’ bila kuweka katika kaburi la sahau ‘Nipe macho nione’ na ‘Umenifanya ning’are’ tambo zake Christina Shusho.

Anaomba Mungu amuongoze kupitia muziki wake atimize azimio lake kuanzisha mradi wa OKOA Youth katika Kaunti ya Homabay ili kukomboa vijana wengi wanaoteswa na virusi vya Ukimwi kupitia nasaha na mafunzo ya Biblia.

Pia analenga kurejea chuoni kusomea shahada ya digrii katika masuala ya biashara. Katika mpango mzima anashauri wasanii wa injili kutoa nyimbo za kujenga wanadamu kiroho ili kujiupesha dhidi ya majanga mengi yanayoendelea kutesa maishani mwetu.

Anadokeza kwamba wasanii wengi hushindwa kupiga hatua katika muziki maana una gharama kubwa hasa kurekodi video nzuri.

Msanii Ogo akiwa katika kazi yake ya ulinzi jijini Nairobi. Picha/ John Kimwere

Pia anaponda maprodusa wale hutumia kazi za wanamuziki wengine kujifaidi bila wahusika kuhusishwa. Anatoa mwito kwa vyuo vya kulinda masilahi ya wanamuziki kuzamia suala hilo zaidi ili kuwaokoa watunzi wengi nchini.

Kadhalika anasema Serikali ina nafasi nzuri kuanzisha mkakati mwafaka ili kuinua wanamuziki wa humu nchini chipukizi wanaokuja.

”Muziki wa Kenya una nafasi kubwa kupiga hatua lakini lazima kazi kubwa ifanye ikiwamo serikali kuwekeza zaidi kama ilivyo katika mataifa yanayoendelea,” alisema. Anasema wasanii chipukizi nyakati nyingi hujipata njia panda huku wengi wakizimwa na wenzao waliowatangulia.