Michezo

John Stones amchoka mke, ajiandaa kuvisha kahaba pete ya harusi

January 21st, 2019 1 min read

NA MWANDISHI WETU

BEKI wa Manchester City na timu ya taifa ya Uingereza, John Stones, 24, amemtema mchumba wake Millie Savage ambaye kwa sasa ni mama wa mtoto wa kike mwenye umri wa miezi 18.

Katika mahojiano yake na gazeti la The Sun wiki jana, Millie alisema Stones anayedumishwa kwa mshahara wa hadi Sh21 milioni kwa wiki ugani Etihad, alimweleza “Yamekwisha. Nataka kuwa huru.”

Kwa mujibu wa Millie, Stones alirejea nyumbani, akakusanya pamoja virago vyake na kuondoka akimwacha pweke katika kasri lao la Sh470 milioni mjini Cheshire, Uingereza mwanzoni mwa wiki iliyopita. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Stones kurudi nyumbani tangu mkesha wa Sikukuu ya Krismasi ya 2018.

Wawili hao walianza kutoka pamoja kimapenzi wakiwa watoto wa umri wa miaka 15. Walikutana kwa mara ya kwanza wakiwa wanafunzi wenye umri wa miaka 12 katika Shule ya Penistone Grammar, South Yorks.

Kulingana na The Sun, Stones amehamia kwa sasa katika chumba cha kukodisha jijini Manchester anakotarajiwa kulipia kima cha Sh840,000 kwa mwezi sawa na kocha Pep Guardiola anayeishi katika kimojawapo cha vyumba vya hoteli ya City Suites.

Kwa mujibu wa Millie, kiini cha Stones kumtupa ni kuwaka upya kwa mwenge wa mapenzi kati ya sogora huyo na kipusa Jessica Peaty aliyekuwa na mazoea ya kumwonjesha asali mnamo 2016 katika hoteli ya Lowry jijini Manchester kwa malipo ya hadi Sh126,000 kwa wiki.

Hata hivyo, Millie alimsamehe mumewe mwanzoni mwa 2017 baada ya beki huyo kuchanja chale za kudumu zenye mchoro wa jina ‘Millie’ kwenye mkono wake.