Habari za Kitaifa

Joho afufua azma yake ya urais

February 14th, 2024 2 min read

NA WINNIE ATIENO

NAIBU Kinara wa Chama cha ODM, Bw Hassan Joho amejitokeza rasmi katika siasa za chama hicho cha upinzani akitangaza hadharani kuwa anapania kuwania Urais mwaka wa 2027.

Alipostaafu ugavana mwaka wa 2022, Bw Joho alisema amemaliza siasa za Mombasa akatangaza kusaka tikiti ya ODM kuwania urais, lakini baadaye akajiondoa na kumuunga mkono kinara wa chama hicho, Bw Raila Odinga.

Akiongea Jumanne akiwa Mombasa, Bw Joho ambaye alikuwa amepotea kwa muda mrefu katika siasa za humu nchini alisema analenga siasa za kitaifa baada ya kukomaa kisiasa.

Hii ni baada ya kushinikizwa na wakazi na baadhi ya wanasiasa wa Mombasa kurudi kwenye ulingo baada ya kuacha siasa za Pwani yatima.

“Nimesikia watu wakisema wanataka nipiganie kiti fulani hapa Mombasa, lakini nataka kuwaambia na munisikize kwa makini kwa masikio mawili. Siasa za Mombasa nilimaliza, kile kiti nitakachopigania ni Urais,” alisema Bw Joho.

Bw Joho ambaye alikuwa Gavana wa Mombasa kwa hatamu mbili alisema mpwani ama mzaliwa wa Mombasa anaweza kuwa Rais wa nchi.

“Nani aliwaambia mzaliwa wa Mombasa hawezi kugombea urais na kuibuka mshindi? Na tena waanze kujipanga manake naskia wengi wanataka kuwa kwenye debe. Nawaambia hapa mchana 2027 niko debeni na waelewe,” alisema Bw Joho.

Alisema chama cha ODM kina demoksrasia.

Bw Joho alisema katika chama cha ODM, Bw Wyclife Oparanya, ni mojawapo ya wanasiasa ambao wanapania kugombea urais. Hata hivyo alisema yuko tayari kulumbana kwenye chama ili atimize malengo yake.

Alisema aliingia siasa alipokuwa kijana mdogo na kusimama kidete na kinara wa ODM Bw Raila Odinga kwa hali na mali bila kumuasi.

“Nilishamfuata na kumwambia aniangalie kwa huruma na kunitawaza kama mgombea wa urais. Nilimwambia aseme Hassan Joho tosha,” aliongeza Bw Joho.

Haya yanajiri siku chache baada ya wanasiasa wa Mombasa kumshinikiza ajitokeze kwenye siasa za Pwani baaada ya eneo hilo kukosa kiongozi shupavu na mwelekeo bora.

Viongozi wa ODM pia wamekuwa wakilalamika namna chama hicho kimekosa uongozi wakimtaka Bw Joho awasaidie kuifufua hasa kwenye zoezi la kusaka wanachama wapya.

Tangazo la Bw Joho limetokea wakati ambapo muungano mzima wa Azimio la Umoja One Kenya unakumbwa na ushindani mkali kuhusu ni nani atakayetangazwa kushindana na Rais William Ruto, katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Wanasiasa wa muungano huo unaojumuisha vyama mbalimbali vikiwemo Wiper, Narc-Kenya, DAP-Kenya, KANU na nyinginezo wameonekana kujigawanya kwa makundi tofauti ambapo kila kundi linashabikia mwanasiasa fulani.

Kwa mfano, kinara wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka amekuwa akishirikiana na mwenzake wa DAP-K, Bw Eugene Wamalwa, ikiaminika wanapanga mikakati ya kumwezesha Bw Musyoka kuwa mgombeaji urais 2027.

Kwa upande mwingine, vyama vya Jubilee na Narc-Kenya pia vimekuwa vikipanga mikakati yao ya kando.

Hata hivyo, Bw Odinga amekuwa akisisitiza kuwa, vyama vyote viko huru kujiimarisha kwa vile hatua hiyo itasaidia pia kuimarisha muungano wao wa Azimio kwa maandalizi ya siasa za 2027.