Habari

Joho ahimiza wakazi wakubali mradi wa ujenzi wa majumba katika mtaa wa Buxton

August 16th, 2020 1 min read

Na WINNIE ATIENO

GAVANA wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho amepiga jeki mradi wa ujenzi wa majumba katika mtaa wa Buxton utakaogharimu Sh6 bilioni.

Mradi huo unaotekelezwa na mfanyabiashara maarufu na mwanasiasa Suleiman Shahbal utasaidia zaidi ya wakazi 500 wanaoishi humo katikati mwa jiji la Mombasa.

Kulingana na Gavana wa Mombasa, wakazi hao watakuwa wamiliki wa majumba hayo.

Hata hivyo, wakazi wengine walipinga mradi huo wakisema hawakuhusishwa.

Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Buxton. Picha/ Winnie Atieno

“Tuna wasiwasi sababu hatukupewa muda wa kutathmini mradi huo. Huwa tunalipa kodi ya nyumba ya vyumba viwili vya kulala Sh3,700 na ile ya chumba kimoja Sh2,800,” alisema Bw Baya Mwanyule.

Wakazi wanaopinga mradio huo walimsihi Bw Joho kufanya kikao cha dharura ili kusawazisha swala hilo.

Mwenyekiti wa kamati ya Buxton, Sheikh Mohammed Khalifa, alisema watapewa fidia ya Sh200,000 kila mmoja.

Akiongea kwenye mkutano na ‘waathiriwa’ wa mradi huo, Bw Joho aliwahakikishia wakazi kwamba watafidiwa.

Ubomoaji esteti hizo unatarajiwa kuanza rasmi hivi karibuni huku ujenzi wa mradi mpya ukitarajiwa kuanza Januari mwakani.

“Tumekuwa katika mkutano na wakazi ambao asilimia 95 wanaunga mkono mradi huo. Ajenda yetu ni kujenga makao bora kwa wakazi. Mradi huu utabadilisha mandhari ya Mombasa na maisha ya wakazi ambao watapewa kipaumbele,” alisema Bw Joho.

Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho. Picha/ Maktaba

Bw Joho alisema mradi huo utahakikisha majumba 1,900 ikiwemo shule, vituo vya vijana na ukumbi wa spoti, yanastawishwa.

“Wakazi watapewa fursa ya kunua majumba,” alisema.

Mmiliki wa mradi huo, Bw Shahbal alisema mandhari ya Mombasa yatabidilika kutokana na ujenzi huo na kufungua nafasi za ajira.

Mmoja wa wakazi wa mtaa wa Buxton akizungumza na wanahabari huku wenzake mtaani humo wakiwepo. Picha/ Winnie Atieno