Joho ajitokeza baada ya muda mrefu, aomboleza kifo cha BBI

Joho ajitokeza baada ya muda mrefu, aomboleza kifo cha BBI

Na VALENTINE OBARA

GAVANA wa Mombasa, Bw Hassan Joho, hatimaye amevunja kimya chake kilichodumu kwa zaidi ya mwezi mmoja, kuhusu matukio ya kisiasa nchini.

Mara ya mwisho alipoongoza hafla ya hadharani ilikuwa katika sherehe za Idd-Ul-Adha mnamo Julai 19, ambayo ilihudhuriwa pia na Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga.

Wiki chache zilizopita, maafisa wakuu wa kaunti hiyo wakiongozwa na Kaimu Katibu wa Kaunti, Bw Joab Tumbo, waliambia maseneta waliotaka kukutana naye kwamba, alikuwa amesafiri nje ya nchi.

Bw Joho ambaye alisemekana alirudi nchini wiki iliyopita, sasa anataka viongozi wawazie upya jinsi urekebishaji wa Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) utakavyofanikishwa.

Kupitia kwa taarifa, Bw Joho alieleza masikitiko yake kwamba BBI ingeleta mafanikio mengi kimaendeleo nchini na kuzimwa kwake ni pigo kubwa kwa taifa.

Kulingana naye, mapendekezo kama vile kuongeza mgao wa fedha kwa serikali za kaunti, ugavi wa fedha za maendeleo kwa wadi, na hitaji la kubuniwa kwa tume ya huduma za afya, ni baadhi tu ya matunda ambayo taifa lingevuna kutoka kwa marekebisho ya Katiba.

“Inasikitisha kuwa Wakenya watalazimika kusubiri muda mrefu zaidi kabla wafurahie haya, yote kwa sababu ya siasa chafu. Huu ni ukweli mchungu unaonikera mno kama Naibu Kiongozi wa ODM na vile vile, kama Gavana wa Mombasa anayefahamu fika kuhusu umuhimu wa ripoti ya BBI,” akasema.

Bw Joho wakati huo huo aliibua gumzo miongoni mwa baadhi ya wananchi kwa kubandika picha mitandaoni iliyoonyesha akiwa pamoja na Naibu Rais William Ruto katika mkutano wa zamani.

Mapema mwaka huu, Mbunge wa Emurua Dikirr, Bw Johanna Ng’eno, alidai mashauriano yalikuwa yanaendelea kumshawishi Bw Joho aungane na Chama cha United Democratic Alliance (UDA).Safari ya urekebishaji wa Katiba iliyoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga, ilipigwa breki na Mahakama ya Rufaa iliyokubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu kwamba mchakato huo ulikiuka sheria.

Baadhi ya sababu zilizotolewa ni kuwa, wananchi hawakuhusishwa ipasavyo katika mchakato huo, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haikuwa na idadi ya kutosha ya makamishna kuidhinisha mpango wa kurekebisha Katiba, na rais hakustahili kuongoza mpango huo kwani jukumu hilo linafaa kuwa la raia.

Hata hivyo, wahusika kadhaa wameelekea katika Mahakama ya Juu kutaka baadhi ya maamuzi hayo yabatilishwe.“BBI ililenga kutoa nafasi ambazo zingenufaisha Mombasa na Kenya kwa jumla. Bado kuna muda wa kuwazia upya jambo hili,” akasema Bw Joho.

Kimya kikuu cha Bw Joho ilikuwa imeanza kuibua gumzo miongoni mwa wafuasi na pia mahasimu wake wa kisiasa.Wakati alipokosekana katika mikutano ya Bw Odinga maeneo ya Pwani, ikiwemo ikuluni Mombasa ambapo rais aliwaita pia vinara wa Muungano wa One Kenya Alliance (OKA), baadhi ya wapinzani wake walidai ameanza kutengwa katika mashauriano ya siasa za kitaifa kuelekea 2022.

Mkutano huo wa Rais Kenyatta na Bw Odinga ulikuwa umehudhuriwa na Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, mwenzake wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, Seneta wa Baringo Gideon Moi, ambaye ni Mwenyekiti wa KANU, mwenzake wa Bungoma Moses Wetang’ula anayeongoza Ford Kenya, na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa ODM.

  • Tags

You can share this post!

Mzee na mwanawe wakamatwa kanisani wakivuta bangi

Waiguru alia kuhangaishwa tena na EACC