Joho ampa Raila masharti makali

Joho ampa Raila masharti makali

Na WACHIRA MWANGI

GAVANA wa Mombasa, Bw Hassan Joho, anataka makubaliano mapya na Kiongozi wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga, kuelekea katika uchaguzi mkuu ujao.

Gavana huyo ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa ODM, ameshikilia kuwa makubaliano yoyote yatakayofanywa kuelekea 2022 lazima yahakikishe kuwa changamoto zinazokumba Wapwani zinatatuliwa katika serikali ijayo.

Akizungumza katika hafla ya tuzo za wafanyabiashara wa Mombasa usiku wa kuamkia jana, Bw Joho, hata hivyo alisisitiza kuwa bado anaunga mkono azimio la Bw Odinga kwa urais.

“Ninamuunga mkono Raila Odinga na nimemwambia kuna mambo ambayo lazima tuangalie upya,” akasema.

Bw Odinga anatarajiwa kutangaza rasmi ikiwa atawania urais, Ijumaa, Desemba 10 jijini Nairobi.

Bw Joho alitoa wito kwa wanasiasa wa Pwani kuungana ili wawe na usemi mmoja wanapotafuta makubaliano na wagombeaji urais.

Kwa sasa, eneo hilo limegawanyika kisiasa wakati ambapo baadhi ya maeneo nchini yameungana kuwasilisha matakwa yao kwa wanasiasa wanaotarajia kuwania urais mwaka 2022.

Baadhi ya wanasiasa wa Pwani waliwasilisha mapendekezo yao kuhusu yale wanayotaka Naibu Rais William Ruto alifanyie eneo hilo endapo atashinda urais.

“Wakati huu tunapoelekea kwa uchaguzi wa kupisha serikali mpya, lazima tuweke kando ubinafsi ili tujadiliane na utawala ujao kuhusu jinsi ilivyo lazima masuala yetu yatatuliwe,” akasema.

Miongoni mwa masuala ambayo yamekuwa tatanishi baina ya serikali ya kitaifa na kaunti za Pwani tangu ugatuzi ulipoanzishwa 2013, ni kama vile ugavi wa mapato ya bandari ya Mombasa, usimamizi wake, na agizo kuwa mizigo yote inayoelekea Nairobi isafirishwe kwa reli ya SGR.

Kisiasa, kumekuwa na mapendekezo kwamba kiongozi anayetoka Pwani apewe nafasi kubwa serikalini kama vile ya naibu rais au waziri wa mamlaka makubwa.

Baadhi ya viongozi hulalamika kuwa Pwani hutengewa tu Wizara ya Utalii tangu zamani.

Hata hivyo, Bw Joho alikwepa masuala tatanishi ya kisiasa na badala yake akaeleza kuhusu mahitaji ya Pwani kiuchumi katika serikali ijayo.

“Ni lazima Mombasa ihesabiwe kama eneo huru kiuchumi. Lazima tuwe na makubaliano. Lazima turudi nyuma na tuangalie upya makubaliano kuhusu SGR,” akasema.

Aliongeza kuwa mwelekeo mpya wa kustawisha utalii utahitajika kwa kurekebisha sera kuhusu safari za ndege ili ndege nyingi za kimataifa ziwe huru kusafiri moja kwa moja hadi Mombasa.

“Ikiwa tunataka kustawi kama eneo kuu la utalii, hatuwezi kuendelea kusihi watu wachache waje kutembelea Mombasa kila mara. Mbona bado tunajadili mambo haya mwaka wa 2021?” akauliza.

Wakati huo huo, kwa mara nyingine alitetea biashara za familia yake za uchukuzi wa mizigo bandarini ambazo zimekuwa zikikashifiwa na baadhi ya mahasimu wake wa kisiasa.

Alisema familia yake inafanya biashara katika Bandari ya Mombasa sawa na wanasiasa wengine na wafanyabiashara ambao hupata kandarasi za serikali kwa njia za haki.

Bw Joho ni mmoja wa magavana watatu wa kaunti za Pwani watakaokamilisha kipindi cha pili cha uongozi mwaka ujao, na wanatarajiwa kutafuta nafasi katika serikali ya kitaifa.

Wengine ni Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya ambaye anaegemea upande wa Dkt Ruto, na mwenzake wa Kilifi, Bw Amason Kingi ambaye hajatangaza mwelekeo atakaochukua kupitia chama chake cha Pamoja African Alliance (PAA).

You can share this post!

Mioto shuleni: Rai wizara ibuni kamati maalum

Wafuasi wa Hasla wakosoa Rais ‘kudai amestawisha kilimo’

T L