Habari Mseto

Joho aongeza ada za kuzika makaburini Mombasa

September 28th, 2019 2 min read

Na WINNIE ATIENO

BAADHI ya wakazi wa Mombasa wameamua kuwa wakichoma maiti badala ya kuizika, baada ya serikali ya Gavana Hassan Joho kuongeza ada ya mazishi katika makaburi ya umma.

Kwenye Makadirio ya Fedha ya mwaka huu wa 2019/2020, serikali ya Gavana Joho inapendekeza kuongeza ada za makaburi yakudumu kutoka Sh25,000 hadi Sh30,000 sawa na ada za ufukuaji wa maiti.

Hata hivyo, ada ya kuchimba makaburi imesalia Sh1500 na ile ya kaburi lisilodumu ikisalia Sh6,500.

Serikali hiyo ina maeneo matatu ya makaburi ya umma ikiwemo Kisauni, Mbaraki na Mayimbo.

Lakini wakazi wamepinga ada hizo za kuzika wapendwa wao wakisema ni kumnyanyasa masikini.

“Kuishi ni gharama kufa nako kuna ada, jamani, twaelekea wapi sisi? Heri tuchome maiti badala ya kuzika kwa kuwa hatuwezi hiyo gharama,?” aliuliza Bi Lydia Ndinda, mkazi wa Changamwe.

Akiongea na Taifa Leo, Bi Ndinda alisema ada ya kuchoma ni nafuu na haina gharama nyingi.

“Lakini tunamsihi gavana wetu atupilie mbali ada hiyo, wacheni roho za maiti zipumzike. Sisi maskini ndio tunaoumia,” aliongeza.

Bw Victor Wesonga, mkazi wa Jomvu, alisema ada hiyo itapelekea maiti nyingi kusalia kwenye mochari kwa sababu zinaongeza gharama kwa familia za marehemu.

“Hii ni kwa sababu huwa tunashindwa kugharamia bei ya mazishi hapa Mombasa. Itabidi tufanye harambee na hiyo bado ni gharama nyingine mwili ukiendelea kukaa katika chumba cha kuhifadhia maiti. Tunaomba ada hiyo ipunguzwe, maiti hana pesa,” alisema.

Malipo

Hata hivyo, mkurugenzi wa mapato, Bi Ramla Mohammed alisema ada hizo ni muhimu ili serikali iweze kulipa wafanyakazi wa maeneo ya makaburini.

Alisema serikali ya kaunti inahitaji fedha ili kutoa huduma kwa wakazi.

Hata hivyo, wakazi walinung’unika wakisema ni unyanyasaji wa hali ya juu katika eneo ambalo uchumi umeathiriwa mno.

Afisa huyo alisema ni mara ya kwanza serikali ya kaunti inaongeza ada hizo.

“Najua mmeshtuka lakini kumbukeni hatujawahi kuongeza ada hizi tangu ugatuzi. Tumeongeza kwa Sh5000 tu,” Bi Mohammed alisema.