Habari

Joho apiga jeki Embrace kwa kuunga juhudi zao

August 31st, 2019 2 min read

Na WACHIRA MWANGI na MARY WANGARI

GAVANA wa Mombasa Hassan Joho amepiga jeki kundi la wanawake la Embrace linalounga mkono muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Akizungumza Jumamosi katika Kaunti ya Mombasa, Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru alimshukuru Gavana Joho kwa kuwa gavana wa kwanza mwanamume kuunga mkono kundi la Embrace ambalo pia linapinga mswada wa kura ya maamuzi wa Punguza Mizigo.

“Ningependa kumshukuru Gavana Hassan Joho. Hatujawahi kwenda mahali pengine na kuwa na gavana mwanamume. Yeye ndiye gavana wa kwanza kuunga mkono Embrace,” alisema.

 

Gavana wa Mombasa Hassan Joho akiwa na mwenzake wa Kirinyaga Anne Waiguru – ambaye pia hupenda kuitwa Anne Kamotho tangu ahalalishe ndoa yake na Wakili Waiganjo Kamotho – katika mkutano wa Embrace Kenya Agosti 31, 2019, uwanjani Tononoka, Mombasa. Picha/ Wachira Mwangi

Bi Waiguru alikariri kuwa wanaunga mkono Rais Uhuru na Kiongozi wa ODM, kwa hatua yao ya kuzima uhasama wao na kuridhiana kupitia ‘handisheki’.

“Nimesimama kama mama kiongozi kusimama na Rais Uhuru na Raila kwa kusalimiana ili Kenya itulie. Kunapokuwa na ghasia kina mama ndio wanaoteseka zaidi kwa sababu uchungu wa mwana aujuae ni mama ndiposa kama kina mama tunasimama kidete na Rais Uhuru na Raila na hatubanduki,” alisema.

Kiongozi huyo wa Kirinyaga pia alisema wakati ulikuwa umewadia kwa Kenya kuwajumuisha watu wa makabila mengine katika uongozi kinyume na kutawaliwa na makabila mawili pekee.

“Nchi imefika mahali ambapo hatuwezi kuwa kila siku ni makabila mawili tu yako katika uongozi. Lazima tupanue pale viti vilivyo pale juu ili tuwe na nafasi ya viongozi kutoka sehemu mbalimbali nchini Kenya,” akasema.

Aidha, aliukashifu mswada wa Punguza Mizigo akisema kinyume na wengi wanavyofikiria, mswada huo haulengi kuwapunguzia mzigo wananchi bali unanuia kupunguza idadi ya viongozi wanawake.

“Tusidanganwye na mswada huu ambao umekuja wa Punguza Mizigo; hilo ni jina tu. Mzigo ambao wanapunguza ni kina mama. Asilimia 60 ya kura hupigwa na wanawake lakini wakati wa kupunguza mzigo wanatoa kina mama katika uongozi wa taifa,” akasema.

Alisema kwamba kundi la Embrace linapigia debe kupanuliwa kwa uongozi wa taifa kwa kuongeza viti vingine vitatu ikiwemo Waziri Mkuu, manaibu waziri mkuu wawili, Rais na Naibu Rais, ili kumaliza mizozo ya uongozi.