Habari MsetoSiasa

Joho ashauri wakazi wajinyime raha msimu wa corona

April 19th, 2020 1 min read

MISHI GONGO na WINNIE ATIENO

GAVANA wa Mombasa Hassan Joho amewataka wakazi waige mfano wake, kwa kujilazimisha kuacha mambo ya burudani, ili wasaidie kudhibiti maambukizi ya virusi vya

Akizungumza nje ya afisi yake alipokuwa akipokea misaada kutoka kwa wahisani, gavana huyo wa kaunti ya pili kwa maambukizi mengi ya corona nchini, alisema anaelewa ugumu wa kujizuia, lakini ndiyo njia pekee kwa sasa.

“Kama mnavyojua, mimi ni mtu ninayependa kutangamana na watu, lakini nimelazimika kubadili mienendo yangu tangu kuingia kwa virusi vya corona, naketi nyumbani,navaa maski kama walivyoagiza maafisa wa afya. Nawaomba wakazi nanyi mfanye hivyo,” akasema.

Aliwaomba wakazi wa Mombasa na Kenya kwa jumla wafuate maagizo ya wizara ya Afya ili kuangamiza janga hilo kwa haraka.

“Nikitoka nyumbani naingia afisini na ninapomaliza shughuli za kazi narudi nyumbani. Sijazoea kukaa nyumbani, nimekuwa mwanasiasa nusu ya maisha yangu. Nimezoea kujumuika na watu mashinani lakini sasa hivi nimebadilika,” akasema Bw Joho.

Gavana huyo alisema kuwa hakutarajia maishani yake kama kungewahi kushuhudiwa janga kama la corona ambalo lingeleta maafa makubwa duniani.

“Tumekuwa tukisoma kuhusu majanga ya maradhi nyakati za nyuma lakini haikuwaikufikia hatua ya baba kutoweza kumkumbatia binti yake. Jana nilipowasili nyumbani kutoka afisini, mwanangu alinikimbilia kwa shangwe lakini sikuweza kumshika kabla ya kujisafisha. Ni jambo la uchungu, lakini tunafaa kukubali kuwa corona iko nchini na tufuate mikakati iliyowekwa kuikabili,” akasema.

Gavana huyo aliwahakikishia wakazi wa Mombasa kuwa iwapo watafuata masharti yaliyowekwa na serikali basi mambo yatarudi kuwa sawa kama zamani.