Joho ashinikiza sera za mizigo bandarini zibadilishwe

Joho ashinikiza sera za mizigo bandarini zibadilishwe

Na WINNIE ATIENO

GAVANA wa Mombasa, Bw Hassan Joho, amehakikishia wakazi na wafanyabiashara katika kaunti hiyo kuwa ataendelea kushinikiza serikali ya kitaifa ipitishe sera ambazo zitasaidia kukuza uchumi wa mji huo.

Bw Joho alilalamika kuwa, sera iliyopitishwa na serikali 2019 kwamba kampuni zote zilizosajiliwa Nairobi ziwe zikisafirisha mizigo yao moja kwa moja kutoka bandarini hadi katika jiji hilo kuu kupitia kwa reli mpya ya SGR imedhuru biashara za vituo vya kuhifadhi makasha ya mizigo Mombasa.

Tangu wakati huo, vituo vingi vya kuhifadhi makasha ya mizigo inayotoka bandarini (CFS) vimefilisika huku vingine vikipunguziwa biashara zao, hali ambayo imesababisha idadi kubwa ya watu kukosa ajira na kaunti pia kupunguziwa mapato yake.

“Tuambiane ukweli, uchumi wa Mombasa uliathirika sana wakati SGR ilipoanzishwa. Waagizaji mizigo ambao nambari zao za biashara zimesajiliwa Nairobi wanalazimika kupeleka mizigo yao hadi kwa bohari la Nairobi,” akasema.

Gavana huyo anayekamilisha kipindi chake cha pili mamlakani alisema ataendelea kusaidia wafanyabiashara ili kusiwe na vikwazo vya uwekezaji katika mji huo.

“Tunataka kufanikisha mandhari ambapo biashara zitakuwa zikiendelea kwa saa 24 ili kuwe na nafasi za ajira kwa vijana wetu,” akasema.

Bw Joho ambaye familia yake inamiliki kituo kikubwa cha kuhifadhi makasha ya mizigo Mombasa alikuwa akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa barabara ya Mbaraki.

Ujenzi wa barabara hiyo itakayosaidia uchukuzi kuelekea bandarini unafanywa na Serikali ya Kaunti ya Mombasa kwa ushirikiano na Serikali ya Uingereza.

Gavana alikuwa ameandamana na Balozi wa Uingereza nchini, Bi Jane Marriott na maafisa wa Mamlaka ya Bandari za Kenya (KPA).

Wadau wengine ambao wamekuwa wakipinga agizo hilo la serikali ni Chama cha Wachukuzi nchini, Chama cha Wafanyakazi wa Bandarini, na wamiliki wa vituo vya kuhifadhi makasha ya mizigo inayotoka bandarini.

Wawekezaji wamelalamika kuwa hatua hiyo ya serikali ilisababisha upungufu wa mizigo ambayo inahitaji kuhifadhiwa Mombasa kabla isafirishwe kwingine na hivyo basi makampuni mengi yakaanza kushindania kiwango kidogo cha mizigo.

Mojawapo ya kampuni kubwa inayotoa huduma hizo imesemekana imelazimika kufuta kazi baadhi ya wafanyakazi wake kwani zamani ilikuwa ikichukua takriban makasha 2,000 lakini sasa imepungua hadi karibu 200 pekee.

You can share this post!

KRA kupiga mnada mizigo iliyoachwa

KIPUTE CHA TIM WANYONYI: Leads United inapigiwa chapuo...

T L