Habari za Kitaifa

Joho atisha kamati ya mahojiano kwa utajiri wake wa Sh2.36 bilioni


WAZIRI Mteule wa Madini na Uchumi wa Majini Hassan Ali Joho Jumapili amefichua kwamba utajiri wake ni Sh2.36 bilioni.

Akihojiwa na Kamati ya Bunge kuhusu Uteuzi, Gavana huyo wa zamani wa Mombasa alisema kuwa utajiri wake mwingi unatokana na nyumba zake pamoja na uwekezaji katika kampuni kadhaa.

Japo familia yake ni tajiri, alifichua kuwa utajiri wake wa kibinafsi, kando na wa familia yake, ni zaidi ya Sh2.36 bilioni.

Joho alisema kuwa utajiri huo unajumuisha mali yake ambayo hajaistawisha, nyumba jijini Mombasa, Vipingo, Nairobi na Malindi.
Vilevile, alisema ana hisa katika kampuni kadhaa.

Gavana huyo wa zamani pia ana hisa katika biashara za familia yake ambazo alisisitiza hazihusiani na biashara za serikali.

“Familia yangu inafanya biashara ya kuuza bidhaa,” alisema Joho ambaye alikuwa Naibu kiongozi wa chama cha ODM.

Hata hivyo, Joho alikariri kwamba iwapo ataidhinishwa kuwa waziri, hataringa na utajiri wake.

Ufahari wa maisha ya Joho

“Ninachotaka kuihakikishia kamati hii tukufu ni kwamba ninathamini mambo fulani ya maisha lakini unapotumikia wananchi, lazima kwanza uwafanye wahisi wewe ni mmoja wao. Kwa hivyo, ninapofanya kazi,  ninapojifurahisha nyumbani, hiyo ni hadithi nyingine. Lakini ninapoenda kwa Wakenya, ninafaa kuwafanyia kazi,” alisema Joho anayefahamika kama Sultan.

Joho alikuwa akimjibu Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wah ambaye alisema utajiri wake ulionekana wazi kwenye mtandao wa kijamii wa Tiktok anakoanika maisha yake ya kifahari.

Aidha, alisema kwamba amemiliki saa kadhaa za thamani ya mamilioni ya pesa hata kabla ya kujiunga na utumishi wa umma.

“Uliuliza kuhusu vito vya thamani lakini nazungumzia saa na nilikuwa nikizivaa hata kabla sijawa mbunge. Najua jinsi ya kusawazisha. Sihitaji kuvaa ili niweze kujionyesha” alisema.

“Ninafurahia kuivaa. Hata asubuhi hii, nilikuwa nikijadili iwapo nivae saa au nisivae. Ulikuwa mjadala mkubwa nyumbani. Nilisema nitaiziba kwa shati langu kwa sababu sihitaji kujionyesha,” aliambia Kamati.

Kabla ya Joho kuhojiwa, ni Waziri Mteule wa Uchukuzi Davis Chirchir aliyeibuka tajiri zaidi kwa kumiliki mali ya thamani ya Sh930 milioni.

Mwenye mali ya thamani ndogo zaidi ikilinganishwa na wenzake ni Waziri Mteule wa Maji, Usafi na Unyunyiziaji Eric Muriithi Mugaa, kijana mwenye umri wa miaka 32 aliyesema utajiri wake ni Sh31 milioni, ambaye pia alisema hamiliki gari.