Habari MsetoSiasa

Joho atuza mama aliyejifunika chupa kuzuia corona

April 2nd, 2020 2 min read

WACHIRA MWANGI na DIANA MUTHEU

GAVANA wa Mombasa, Ali Hassan Joho, Alhamisi alimsaidia mwanamke aliyepigwa picha akiwa amekata chupa ya plastiki na kuivaa usoni kama barakoa ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Akiandamana na Kamishna wa kaunti hiyo, Bw Gilbert Kitiyo. Bw Joho alimkabidhi Bi Sisan Kageha Sh100,000 kwa kuwa raia anayejali.

Wawili hao ambao wanasimamia kamati ya Dharura ya Kaunti kuhusiana na janga la corona, walimsifu Bi Kageha kwa kuonyesha mfano mzuri na nia ya kutokomeza maradhi hayo.

“Tulimuona mama na bintiye siku mbili zilizopita akivuka feri huku amejifunga chupa ya plastiki usoni. Niliguswa sana. Kinachofurahisha ni kuwa, mama huyo anazingatia na kuthamini juhudi za kukabiliana na kusambaa kwa maradhi haya hatari,” akasema Bw Joho.

Alimgeukia mwanamke huyo ambaye ni mkazi wa mtaa wa Bomani, Likoni na kumwambia, “Hata kama ulivaa chupa ulikuwa unatuma ujumbe mzito kwa watu kwamba, ipo haja ya kujichunga. Huo ndio ujumbe ambao sisi tumekuwa tukiutoa kila siku. Ulitaka kulinda maisha yako, ya wanao na jamii unayoishi nayo,” akasema Bw Joho.

Mama huyo ambaye kazi yake ni kuuza maji, alisimulia Taifa Leo jinsi alivyokuwa na wakati mgumu kuamua kama ajinunulie vitambaa hivyo vya kuziba pua na mdomo kwa ajili yake mwenyewe na wanawe wawili au anunue chakula.

“Kwa vile sikuwa na pesa za kutosha yote mawili, nilikata chupa ya maji na nikatengeza kitu cha kunizuia kuambukizwa,” akasema, huku akimshukuru Bw Joho kwa kumtambua.

Gavana Joho aliamuru mama huyo apewe barakoa nyingi ili zingine awagawie majirani zake.

“Ni muhimu ukae nyumbani kwa usalama wako na wa watoto wako,” akasema.

Wakati huo huo, kaunti ya Mombasa imepata msaada wa vifaa vya thamani ya Sh60 milioni vya kuwasaidia wagonjwa wa virusi vya corona kupumua. Akizungumza jana, Bw Joho alisema wamepata vifaa hivyo kumi kutoka Uarabuni.

Dkt Iqbal Khandwala ambaye ni msimamizi wa hospitali Kuu ya eneo la Pwani (CGPH) alisema kuwa tayari walikuwa na vifaa kama hivyo 12. Kwa jumla kaunti ya Mombasa ina vifaa 30 vya kuwasaidia wagonjwa wa virusi vya corona kupumua.