Habari MsetoSiasa

Joho aungama SGR inaangamiza uchumi Pwani

September 18th, 2019 2 min read

Na ANTHONY KITIMO

GAVANA wa Mombasa Hassan Joho, hatimaye amevunja kimya chake cha muda mrefu kuhusu athari za reli mpya ya SGR kwa wakazi wa Pwani, na kuelezea masikitiko yake kuhusu jinsi wakazi wengi wameanza hata kushindwa kulipa kodi ya nyumba baada ya kupoteza ajira za usafirishaji mizigo.

Kulingana na Bw Joho, hali ya uchumi imekuwa mbaya kwa wakazi wa Mombasa huku idadi ya watu wanaohama mji huo ikiripotiwa kuongezeka maradufu.

Bw Joho alisema baadhi ya wakazi waliopoteza ajira tangu SGR ichukue nafasi ya kusafirisha mizigo badala ya malori, siku hizi huomba wanasiasa fedha za matumizi ikiwemo kodi ya nyumba.

“Athari za ukosefu wa kazi zimeanza kudhihirika kwa kuwa idadi ya nyumba zinazokosa wapangaji imeongezeka huku wengine wakitufuata sisi wanasiasa wakiomba kulipiwa kodi ya nyumba,” alisema Bw Joho.

Baadhi ya viongozi walioungana na Bw Joho kutoa kauli zao ni pamaoja na seneta wa Mombasa Mohammed Faki, wabunge Omar Mwinyi (Changamwe), Mishi Mboko (Likoni), Zulelakh Hassan (Kwale) na viongozi wengine wa kisiasa.

Wakati huo huo, viongozi hao waliomba serikali kuu kushirikisha kaunti zingine nchini kuhakikisha deni la reli mpya ya kisasa limelipwa kwa wakati badala ya kuachia Wapwani mzigo huo.

Bw Joho alisema mradi huo unafaidi kila mmoja nchini, hivyo basi wote wanapaswa kuhusishwa ili deni hilo liweze kulipwa kwa haraka.

“Wafanyibiashara wanalazimika kulipa asilimia 1.5 ya mapato ya kila mzigo wanaoagiza hivyo tunapendekeza serikali kuu kutafuta njia mwafaka ya kuhakikisha kila anayefaidi na mradi huo anashirikishwa kulipa deni hilo,” alisema Bw Joho.

Wiki iliyopita, ripoti maalumu iliyotolewa na Chuo Kikuu cha Nairobi na kukabidhiwa gavana huyo na viongozi wengine kutoka mkoa wa Pwani ilionyesha hali ya uchumi mkoani Pwani inazidi kuzoroteka huku serikali kuu ikikosa kupata zaidi ya Sh126 bilioni kufuatia amri ya serikali kubeba mizigo yote kwa kutumia reli ya kisasa ya SGR.

Katika ripoti hiyo, asilimia 60 ya wafanyikazi waliokuwa wakihudumu katika mabohari ya mizigo (CFS) wamefutwa kazi huku madereva wa matrela wakithirika kiasi kikubwa.