Siasa

Joho awapongeza Raila na Uhuru

March 11th, 2018 1 min read

CHAMA cha ODM kimeunga mkono mkutano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wake Raila Odinga kikisema hatua hiyo itaipalilia umoja na kufanikisha maendeleo nchini.

Naibu kiongozi wa chama hicho Ali Hassan Joho pia alitaja hatua hiyo kama ya kijasiri na itasaidia kuondoa tofauti za kikabila, kidini na kisiasa ambazo zilikuwa zikisababisha migawanyiko na uhasama nchini.

“Kwa niaba yangu kama Naibu Kiongozi wa chama cha ODM na kwa niaba ya kaunti muhimu ya Mombasa, ningependa kuwapongeza Mheshimiwa Uhuru Kenyatta na Mheshimiwa Raila Odinga kwa kudhihirisha ujasiri, uzalendo na uongozi na kuweka kando tofauti zao jana (Ijumaa) kwa ajili ya Kenya,” akasema  kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Akaongeza: “Nakubaliana na kauli ya viongozi hawa wawili kwamba taifa letu lilikuwa limegawanyika kwa misingi ya kisiasa, kidini na kikabila na huu ni wakati wa kuchukua uamuzi wa kijasiri ili kuokoa meli ya Kenya ambayo imekuwa ikibiliwa na mawimbi makali.”

Bw Joho ambaye ni mwandani wa karibu wa Bw Odinga aliwataka Wakenya wote kuunga na viongozi hao wawili katika jitihada zao za kurejesha Kenya katika mkondo wa maendeleo.

Hii ni kwa sababu, akasema, mageuzi na maendeleo ambayo Wakenya wanapigania yatapatikana tu ikiwa “tutakubaliana kama Wakenya”.